Baada ya kumtambulisha Kiungo Mshambuliaji Ladack Chasambi kutoka Mtibwa Sugar kujiunga nao kwa mkataba wa miaka mitatu, Klabu ya Simba SC imefunguka kuhusu taarifa zinazomhusisha Kiungo wao Mshambuliaji, Willy Essomba Onana, kutakiwa na JS Kabylie ya Algeria.
Katika taarifa ya klabu hiyo jana, ilieleza kuwa imefanikiwa kumsajili Chasambi kwa mkataba wa miaka mitatau na tayari amejiunga na wachezaji wenzake waliopo Zanzibar kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi.
Lakini pia kutokana na taarifa zilizozagaa kuwa Klabu ya JS Kabylie ya Algeria ipo katika mazungumzo na Simba SC kuhusu kuhitaji huduma Onana, Uongozi wa miamba hiyo ya Mtaa wa Msimbazi jijini Dar es salaam umesema, haujawahi kupokea ofa wala simu kuhusiana na suala hilo.
Taarifa hizo zilizagaa mitandaoni zikieleza kuwa JS Kabylie wameonesha nia ya kutaka kumsajili nyota huyo wa Simba SC kutoka Cameroon ili kwenda kuchukuwa nafasi ya Simon Msuva ambaye waliachana naye hivi karibuni.
Meneja ldara ya Habari na Mawasiliano Simba SC, Ahmed Ally, amesema hajapokea taarifa zozote kutoka kwa viongozi wake kuhusu klabu hiyo kupeleka ofa ya kutaka huduma ya Onana.
Amesema kulingana na hali ilivyo kwa sasa hawawezi kumtoa mchezaji yeyote kipindi hiki, kwani wanaendelea kukijenga kikosi chao na mchezaji huyo ataendelea kuwa sehemu ya kikosi cha timu hiyo kwa kipindi chote cha msimu huu hadi mwishoni wa mkataba wake.
“Kwa sasa Onana ni mali ya Simba SC hakuna ofa iliyofika mezani kwetu kutoka JS Kabylie, kwa sasa sio rahisi kumtoa mchezaji ambaye ameingia katika mfumo wa mwalimu, tunaongeza watu kuboresha timu yetu,” amesema Ahmed.
Amesisitiza kuwa baada ya kutambulishwa kwa wachezaji watatu ambao tayari wamewasajili bado wanaendelea kushusha vifaa vipya walivyovisajili kipindi cha Dirisha Dogo ikiwa ni sehemu ya maboresho ya timu yao.
Ameeleza kuna usajili unaendelea kufanyika na wanatarajia kutambulisha nyota wawili ndani ya juma wiki kulingana na mapendekezo ya Benchi la Ufundi linaloongozwa na Kocha Abdelhak Benchikha.