Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya Guinea Bissau, Baciro Cande amesema kuwa anataka kutinga hatua ya mtoano ya Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’ baada ya timu yake kuwasili mjini Abidjan kwa ajili ya mashindano hayo.

Hiyo imekuwa timu ya pili kuwasili katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi kwa ajili ya kushiriki fainali za 34 za Kombe la Mataifa ya Afrika wakati walipotua katika kiwanja cha ndege cha Felix Houphouët-Boigny kwa ajili ya mashindano hayo.

Kocha Cande na timu yake walipokewa na ngoma za asili za Ivory Coast pamoja na mashabiki kibao waliokusanyika kwenye kiwanja hicho cha ndege wakati wakijiandaa kuwakabili wenyeji Jumamosi.

Timu hiyo imepangwa katika Kundi A na inatarajia kukutana na changamoto kubwa kutoka kwa Nigeria na Guinea ya Ikweta katika kundi hilo.

Gunea Bissau inashiriki mashindano hayo kwa mara ya nne na watacheza mchezo wa ufunguzi Jumamosi dhidi ya wenyeji katika mchezo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Olimpiki wa Alassane Ouattara.

Mchezo huo wa ufunguzi wa Jumamosi utakuwa ni mara ya pili kwa Guinea-Bissau kufungua dimba katika mashindano hayo baada ya kwa mara ya kwanza kufungua dimba katika fainali za mwaka 2017 zilizofanyika Gabon huku kocha Cande akiwa katika benchi la timu hiyo.

“Nina uzoefu na mechi za kwanza, katika fainali zangu za kwanza za mashindano haya, tulicheza mchezo wa ufunguzi dhidi ya Gabon na tulitoka sare (1-1).

“Najua Ivory Coast ni timu yenye nguvu kuliko Gabon, lakini Guinea Bissau itafanýya kazi yake, taratibu,” alisema Cande katika mahojiano baada ya timu hiyo kuwasini mjini Abidjan.

Katika Kundi A timu hiyo imepangwa pamoja na wenyeji Ivory Coast, Nigeria, na Guinea ya Ikweta.

Guinea-Bissau itakabiliana na Guinea ya Ikweta katika mchezo wa pili uliopangwa kufanyika Januari 18, 2024, katika Kundi A.

Timu hiyo itakamilisha mechi zake za makundi kwa kucheza na timu nyingine ngumu ya Nigeria katika mchezo utakaofanyika Januari 22 kwenye Uwanja wa Felix Houphouët-Boigny jijini Abidjan.

Nice yamng'ang'ania Jean-Clair Todibo
Ahmed Ally: Hatujapokea ofa yoyote