Kocha wa muda wa Kagera Sugar, Marwa Chamberi amesema kuongeza wanatarajia wachezaji wasiozidi watatu kwenye dirisha dogo la usajili ili kuimarisha kikosi chao.

Kocha huyo amesema nafasi ambazo wamezilenga kwenye usajili huo ni viungo wawili pamoja na mshambuliaji mmoja.

“Lengo letu ni kuongeza wachezaji wasiozidi watatu kwenye dirisha dogo, tunajua siyo kazi rahisi kupata mchezaji mwenye ubora kipindi hiki lakini tutaangalia tukifanikiwa itakuwa vizuri na kama tutakosa siyo mbaya sababu tuna wachezaji wengi kwenye kikosi chetu,” amesema Chamberi.

Aidha, kocha huyo ambaye ameachiwa mikoba ya Mecky Maxime aliyefutwa kazi wiki tatu zilizopita, amesema timu hiyo tayari imeanza mazoezi kwa ajili ya kumalizia mechi mbili zilizobaki kwenye mzunguko wa kwanza Ligi Kuu Tanzania Bara.

Amesema anajua timu hiyo haipo nafasi nzuri na wana mlolongo mbaya wa matokeo na atakachokifanya yeye na wasaidizi wake ni kuimarisha sehemu zenye mapungufu, ili kufanya vizuri na kubadili mwenendo wa timu hiyo.

Kagera Sugar ipo nafasi ya 14 kwenye msimamo wa Ligi Kuu, ikikusanya pointi 13 katika idadi kama hiyo ya mechi walizocheza.

Arteta: Arsenal tunajitafuta upya
De Bruyne ausuuza moyo wa Guardiola