Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali inakaribia kumaliza ujenzi wa madarasa 5,000 kuondoa zamu mbili kwa wanafunzi nchi nzima na kubakisha zamu moja.
Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo alipofungua rasmi Skuli mpya ya Sekondari Tumekuja iliopo Mwembeladu Wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi hii leo Januari 9, 2024 katika shamrashamra za Miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Skuli hiyo mpya ya Tumekuja ina uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,755 kwa wastani wa uwiano wa wanafunzi 45 kwa darasa moja, tayari wanafunzi wameshapangwa wiki ijayo kuanza masomo.
Elimu ni kipaumbele namba moja – Dkt. Mwinyi
Amesema, Serikali itaendelea kujenga maghorofa katika sekta ya elimu kwa wanafunzi kutozidi 45 kwa darasa moja na kufanya uamuzi sahihi kwa faida ya nchi na kuyakarabati majengo ya mji mkongwe.
Aidha, Rais Dkt.Mwinyi pia amesema mafanikio yaliyopatikana katika elimu ni kwa juhudi za Waalimu kwa kuongeza idadi ya ufaulu ikiwemo kutoka wanafunzi 2,000 hadi 6,000 Skuli za Msingi na matokeo ya kidato cha sita ya mwisho ufaulu wa daraja la kwanza hadi daraja la tatu kwa asilimia 90.