Mshambuliaji wa Singida Fountain Gate, Elvis Rupia amesema ushindani uliopo kwenye Ligi Kuu ya Tanzania Bara, umekuwa chachu ya kiwango chake kuongezeka.

Mshambuliaji huyo aliyejiunga na timu hiyo mwanzoni mwa msimnu huu akitokea Polisi FC ya Kenya amesema kwa kipindi kifupi alichokuwa nchini amekumbana na upinzani mkali kiasi cha kushindwa kutamba kama alivyokuwa kwao.

“Ligi ya Tanzania imeipita ligi ya Kenya kwa vitu vingi kuanzia malipo, ushindani wa timu lakini hata kwa upande wa mashabiki kujitokeza uwanjani kuzipa sapoti timu zao, hili ni jambo zuri linaongeza hamasa kwa mchezaji,” amesema Rupia.

Mshambuliaji huyo ambaye alikuwa nje kwa miezi miwili kutokana na majeraha, amesema anatarajia kurudi kwa kasi kwenye mechi za ligi lengo likiwa ni kuifungia timu yake mabao ya kutosha ili kuwania ubingwa msimu huu.

Amesema anatambua haitakuwa kazi rahisi kutokana na ubora wa timu za Young Africans, Simba SC na Azam FC lakini atapambana kwa kushirikiana na wachezaji wenzake kuhakikisha Singida FG inafanya vizuri na yeye kuibuka mfungaji bora msimu huu.

Tangu ajiunge na timu hiyo Rupia amefunga mabao sita katika mashindano yote ikiwemo mawili ya Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho bao moja na Kombe la Mapinduzi mabao matatu.

SMZ yapanga kuondoa zamu mbili za Wanafunzi
Arteta: Arsenal tunajitafuta upya