Timu ya Geita Gold iko hatua za mwisho kukamilisha usajili wa nyota wa zamani wa Kagera Sugar, Erick Mwijage katika dirisha hili dogo la usajili, ikiwa ni pendekezo la pili la kocha mkuu mpya wa kikosi hicho, Denis Kitambi.
Mwenyekiti wa timu hiyo, Leonard Bugomola amesema tayari mazungumzo na baadhi ya wachezaji wapya watakaowasajili yameshaanza na muda wowote kuanzia sasa wataweka wazi majina ya wale waliofikia makubaliano.
“Kwa sasa ni mapema sana kuzungumzia suala la Mwijage, ila kama litakuwepo basi mashabiki wetu tutawafahamisha” amesema Bugomola.
“Malengo yetu ni kufanya vizuri msimu huu hivyo tutasajili kwa matakwa ya benchi la ufundi na sio kusajili tu.”
Kwa upande wake, Kitambi amesema alishawakabidhi ripoti viongozi wa timu hiyo kwa ajili ya kuboresha maeneo yaliyokuwa na mapungufu hivyo kwa sasa asingependa kueleza kwa kina hadi atakapoona wamesajiliwa.
Hata hivyo, imefahamika kuwa tayari nyota huyo aliyeachana na timu ya West Armenia baada ya kuvunjiwa mkataba yupo nchini kukamilisha dili la miaka miwili, akiungana na mshambuliaji Ramadhan Kapera aliyetua akitokea Mbeya Kwanza inayoshiriki Ligi ya Championship.
Kapera aliyeonyesha kiwango kizuri na Mbeya Kwanza akifunga mabao tisa ndiye usajili wa kwanza katika kikosi hicho kwenye dirisha hili akitarajiwa kuendeleza makali aliyotua nayo.