Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida Kamishina Msaidizi wa Polisi, Stella Mutabihirwa amewataka Wazazi kuhakikisha wanakuwa karibu na watoto wao, ili kuwapa malezi bora jambo ambalo litapunguza vitendo vya ukatili kwa watoto na ongezeko la watoto wa mitaani.

Ameyasema hayo wakati akitoa elimu kwa wazazi kwenye Kliniki ya watoto katika Kituo cha Afya cha Sokoine, kilichopo kata ya Misuna na kudai kuwa malezi bora kwa mtoto hayawezi kupatikana kwa wazazi kuacha watoto wao kulelewa na watu wengine, kwa visingizio vya kuwa na kazi nyingi.

Amesema, “Wazazi naomba mnisikilize kwa makini na tena mfahamu kuwa vitendo vya ukatili katika familia vinafanywa na watu wa karibu na familia. Hivyo unapokuwa karibu na mtoto utamjengea uhuru wa kukuelezea mambo mbalimbali yakiwemo vitendo vibaya alivyotendewa na wenzake ama mtu yeyote. Ili tuweze kuwaweke watoto huru lazima tujenge tabia ya kuongea na watoto wetu na sio na kuwaachia wadaidizi wa ndani peke yao kutulelea watoto wetu.”

Kwa upande wake Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Singida, Mkaguzi wa Polisi Amina Abdallah amewafundisha Wanawake hao juu ya madhara ya ukatili katika familia, ambayo hupelekea watoto kuathirika kisaikolojia na kutotimiza ndoto zao za kimaisha.

Naye Daktari kutoka Zahanati ya Polisi Mkoa wa Singida, Sgt. Salumu Mizungu amewataka wazazi hao kuachana na mila na desturi zilizopitwa na wakati, ikiwemo vitendo vya ukeketaji wa watoto wa kike kwani vinaweza kupelekea kupata maambukizi ya magonjwa na hata kupelekea kupoteza maisha.

Jaji Mkuu alitahadharisha Taifa, amuandikia barua Rais
Wizara yawatahadharisha Wananchi uwepo 'Red Eyes'