Heldina Mwingira.

Ukatili dhidi ya Wanawake Mtandaoni unaweza ukatokea kwa namna nyingi, ikiwemo kutumia picha za utupu au video za utupu kama kulipiza kisasi na  kutumia maneno yasiyo na staha yaani matusi na kejeli kwa jinsia ya kike kwa kujua aama kwa kutokujua.

Wahusika  ambao wanafanya ukatili huo wanaweza kuwa wenza wa sasa au wa zamani, watu wanaofanya kazi pamoja, waliosoma katika shule moja, ndugu, marafiki na watu binafsi.

Baadhi ya Watu ambao huathirika mara kwa mara kama vile watetezi wa haki za Wanawake, Waandishi wa Habari, Wasanii, watu mashuhuri na Wanasiasa, ambapo ukatili huu dhidi yao huwa na madhara mbalimbali kwao na kwa jamii inayowazunguka

Matukio kama haya hupelekea Wanawake kupata sonona, kutengwa, woga, aibu, hatia, kupata wasiwasi, na kujitenga na wakati mwingine kuna uwezekano wa  kuwa na mawazo ya kutaka ama kujia.

Kutokana na utafiti uliofanywa na Watetezi wa haki za wanawake (WHRDs), unasema aina za athari za kisaikolojia zinazopatikana ni Unyogovu, wasiwasi, wasiwasi kushiriki katika jamii anayoishi, na  kujisikia huzuni.  Pia utafiti huo unaonesha  kuwa wanawake wengi walipata ugonjwa wa mfadhaiko baada ya kiwewe (PTSD), kutokana na ukatili dhidi yao.

Mmoja wa wathirika  aliripoti hisia za paranoia baada ya kufanyiwa ukatili na alisema kuwa alipata tabia ya kuhuzunisha ambayo iliharibu afya yake ya akili na ilichukua muda kukabiliana nayo hali hiyo akisema, “nilihisi kuchanganyikiwa na kukosa usingizi, kujilaumu, kutojiamini, aibu, na unyonge.’

Kutokana na changamoto hiyo ya ukatili dhidi ya Wanawake Mtandaoni, Dar24 Media ilimtafuta Mwanasaikolojia mbobevu, Paul Mashauri ambaye alitoa ufafanuzi kuhusu tafsiri ya ukatili dhidi ya wanawake mtandaoni.

Alisema, “ukatili wa wanawake mtandaoni hauna tafsiri moja na kwa kuutambua bali inategemeana na tamaduni ya jamii husika, mfano kule jangwa la Kalahari ikichapisha picha ya Mwanamke kwenye mitandao ya kijamii ambayo inaonesha matiti yako wazi, kwa upande wao ni kitu cha kawaida kwa sababu utamaduni wao unaruhusu kuvaa hivyo, ila kwa nchi nyingine za Afrika kama Tanzania ukichapisha picha zenye maudhui ya hivyo ni ukatili.”

Alisema, mara nyingi watu walioathirika kisaikolojia, hutafuta au kutafutiwa ushauri wa kitaalamu ambao humsaidia mwathiriwa mchakato na kukabiliana na athari za kisaikolojia na Wataalamu wa Saikolojia kama mwongozo na nyenzo za kumsaidia mwathirika kupona na kujenga ustahimilivu.

Aidha, Mashauri aliongeza kuwa katika kumtibia mtu aliyeathirika kisaikolojia kutokana ukatili dhidi ya Wanawake mtandaoni inabidi uangalie yuko katika hatua gani, kwa maana kuna hatua mbili katika kuathirika kisaikolojia na kila mtu hutibiwa kutokana na hatua aliyofikia.

‘Kuna hatua ya awali, katika hatua hii muathirika anapata mshtuko na kutoamini kama imetokea, anakuwa na hasira na  tiba ya hatua hii ni mwathirika kupata unasihi na kwa  kumsaidia unamtafutia kundi la watu walipata changamoto ya ukatili kama yeye ili aweze kujua yeye sio wa kwanza na asione dunia imeisha  na litapita tu,” alisema.

Anasema akiwa ameathirika katika hatua ya pili, uwezo wa akili yake hupata shida, kwa hatua hii huwa anajichukia na hata akijiona kwenye kioo hujiona hafai, huwa na sonona na mfadhaiko baada ya kiwewe na anaweza kufanya kitu ambacho hata yeye mwenyewe hajui kama anafanya na anapoteza kumbukumbu.

Katika hatua hii inabidi atafutiwe mtu wa karibu ili awe anamsaidia, anaongea nae na anamuangalia ili aweze kuendana na mazingira ila pia hali ikizidi muathirika anatakiwa atibiwe na  mtaalamu wa tiba ya akili na sio mnasihi.

Hata hivyo, Mitandao ina faida nyingi kwa Wanawake inaboresha maisha ya Wanawake kwa kuwawezesha na maarifa, upatikanaji wa habari na fursa ila ni muhimu kuitumia ipasavyo ili kuepuka changamoto za kisaikolojia ambapo Paul Mashauri  anasisitiza kuwa mtu yeyote anapojiunga katika mitandao ya kijamii lazima aweke mipaka yake kwani hazuiwi cha kufanya ila kuna sheria  zinazomdhibiti.

Kisaikolojia, Wanawake hujisikia vizuri na wenye furaha kwa kuwa huru kuelezea vitu vyao mtandaoni kwa namna mbalimbali, hivyo ukimnyima nafasi ya kuwa huru ni kumuharibia muundo wake wa maisha na kumnyima asili yake.

Nigeria haitaki kurudia makosa - AFCON 2023
PSG yamtega Kylian Mbappe