Na Humphrey Edward.

Mwaka 1993, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilitoa azimio la kutokomeza ukatili dhidi ya Wanawake, likisema matukio ya unyanyasaji dhidi yao husababisha madhara ya kisaikolojia na kunyima uhuru, huku ukiwekwa msisitizo kwa kutenga siku ya Kimataifa ya kutokomeza ukatili dhidi ya Wanawake Novemba 25, ambayo inaenda sambamba na siku 16 za harakati za kutokomeza ukatili huo na kufikia kilele chake Desemba 10, ambayo ni siku ya Haki za Binadamu Duniani.

Umoja huo, ulisema matukio ya ukatili dhidi yao pia huwaathiri Wanawake katika hatua zote za maisha yao, ikiwemo kielimu na kimaisha kiujumla, huku ikitambulika kwamba unyanyasaji huo wa kijinsia huweza kutokea kwa mtu yeyote, mahali popote, lakini Wanawake na wasichana wako hatarini zaidi, hasa kwa wasichana wadogo na wanawake watu wazima.

Kibaya zaidi inaarifiwa kuwa zaidi ya Wanawake au Wasichana watano huuawa kila saa huku, mwanamke mmoja kati ya watatu akiwa amewahi kufanyiwa ukatili wa kimwili au wa kingono angalau mara moja katika maisha yake na asilimia 86 ya wanawake na wasichana wanaishi katika nchi zisizo na ulinzi wa kisheria dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia ikiwemo ule wa mitandaoni.

Ukatili wa Mtandaoni dhidi ya Wanawake hufanyika kwa njia mbalimbali, kama vile kusambaza picha za utupu bila ridhaa, kuaibisha miili, matusi nk.

Lakini upo ukatili wa Wanawake mtandaoni ambao hufanywa na baadhi ya Vyombo vya habari kwa njia mbalimbali, kama vile kuchapisha picha au kuendeleea kusambaza picha za utupu, zisizo na maadili nk.

Pia, Vyombo hivyo hutumia vichwa vya habari na picha za namna hiyo au uhalisia wa matendo ya mwathiriwa baada ya muhusika (mtendwa) kuhojiwa maswali yenye tafsiri ya fedheha.

Tafiti.

Utafiti uliofanywa na DW Akademie 2023, juu ya  namna ya kuripoti ukatili dhidi ya Wanawake mtandaoni Afrika mashariki, umeainisha kuwa Vyombo vya Habari vimekuwa na ukatili dhidi ya jinsia hiyo mtandaoni.

Kibaya zaidi, utafiti huo umeonesha kuwa Tanzania imekuwa ikifanya ukatili dhidi ya Wanawake kwa aina tano ambazo ni kuaibisha mwili mtandaoni, uonevu mtandaoni, kuchapisha na kutuma picha za utupu bila ridhaa, ufuatiliaji mtandaoni taarifa binafsi bila ridhaa na ufuatiliaji mienendo ya mtumiaji kwa nia ya kudhuru.

Kwa utafiti huu, bila shaka Wanahabari wengi hawafahamu vizuri kuhusu maana na vitendo vinavyoashiria ukatili dhidi ya wanawake mtandaoni kutokana na ushamiri wa matukio hayo kwa jamii na sio kupungua kwani kwasasa kila kukicha utasikia ripoti ya mattukio hayo kama aina fulani ya mambo ya kileo na mengi yanaonekana kuwa ni ya kawaida.

Hili likailazimu Dar24 media kuzungumza na Mwandishi wa chombo kimoja cha Habari nchini (Jina linahifadhiwa), ambaye alisema ukatili mtandaoni umekuwa upande wa Wanawake na mara nyingi ukisababishwa na waathirika wenyewe kupenda umakini kutoka kwa watu.

Alisema, “wanataka kiki na kutambulika katika jamii. Wanahabari wanachapisha kitu ambacho wao wenyewe Wanawake wamechapisha katika akaunti zao binafsi, kwa hiyo mimi sichukulii kama ni shida. Neno ukatili limekuwa kubwa na lenye utata na kwanini lisiwe uvunjifu wa maadili badala ya ukatili?.”

Ni wazi kuwa ukatili dhidi ya wanawake unaendelea kuwa kikwazo katika kufikia usawa, maendeleo, amani pamoja na utimilifu wa haki za binadamu ikiwemo za Wanawake na Wasichana. Na ahadi ya Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), ya kutomuacha mtu nyuma hayawezi kutimizwa bila kukomesha ukatili dhidi yao.

Dhihirisho.

Ni wazi maoni ya Mwandishi huyu yanadhihirisha kuwa uelewa finyu kuhusu ukatili dhidi ya Wanawake mtandaoni hupelekea Wanahabari kuwa sehemu ya ukatili huo kutokana na mifano mingi iliyo hai na inayojidhihirisha.

Wengi wamekuwa ni sehemu ya kuendeleza ukatili huo ama kwa kuelewa ama kwa kutoelewa kwani huendeleza kuuchapishaji wa habari zenye makosa ya kiunyanyasaji wakihisi wanaelimisha ama kuutarifu umma kihabari, hali wanakuwa sehemu ya unyanyasaji huo.

Mfano, Desemba 2023 chombo kimoja cha Habari za Mtandoni kilichapisha picha ambayo inamuonesha Mwanamke akiwa amevaa mavazi na akiwa katika pozi la utata na alipoulizwa akajibu kuwa alikuta imechapishwa katika akaunti binafsi ya huyo Mwanamke.

“Alichapisha mwenyewe kwenye akaunti yake akiwa na vibe na mood ya furaha kisha sisi tukaichukua na kuifanya habari yetu katika chombo chetu cha habari,” alijitetea Mwandishi huyo.

Hii inathibitisha kuwa bado uelewa dhidi ya wanahabari na kuchukulia ukatili dhidi ya wanawake mtandaoni ni kitu cha kawaida na ni dhahiri kuwa suala la ukatili linaweza kuanzia akaunti za binafsi za watu na kuwekwa katika akaunti za Vyombo vya Habari.

Lakini pia zipo kesi kadhaa ambazo ziliwahi kuripotiwa zikionesha namna ambavyo unyanyasaji wa Wanawake mtandaoni ambapo Binti mmoja alijikuta katika wakati mgumu baada ya picha zake za faragha kusambazwa na rafiki yake ambaye inadaiwa aliziuza katika mitandao ya Ngono huko mataifa ya Ulaya na hivyo kupelekea wanaharakati kumpa msaada wa kisaikolojia na akaunti za mtandao huo kufungwa.

Aidha, kwa hapa nchini tuliwahi kusikia kesi kadehaa ambazo si vyema kuzitaja kwa kulinda majina ya wahusika na kujali maadili husika ya vyombo vya Habari ambayo yaliweza kuleta fedheha kwa familia za wahanga na hata muhusika mwenyewe na kazi zake kiujumla, mambo haya yanapaswa kukemewa vikali kwani yanaathiri nguvu kazi ya Taifa na afya za wahusika.

 

Inawezekana ikizingatiwa

Hata hivyo, Vyombo vya Habari vinaweza kuripoti juu ya mada ya ukatili bila kuendeleza ukatili dhidi ya wanawake, vile vile katika kuripoti kesi za ukatili wa wanawake mtandaoni inabidi wanahabari wazingatie yafuatato:

1. Lugha sahihi

Kutumia lugha sahihi wakati wa kutoa taarifa kuhusu ukatili wa dhidi ya Wanawake kwenye vyombo vya habari na Misamiati inayohusiana na ukatili huo mitandaoni ambayo inaendelea kubadilika, hivyo Mwandishi asipokuwa makini hujikuta amehusika katika ukatili.

2. Matumizi ya Maneno

Kuhakikisha maneno yanayotumika yasiwe sababu au muendelezo wa ukatili kwa wanawake mtandaoni kwani wengi wamejikuta wakiandika au kuchapisha maneno bila kujua tafsiri halisi ya neno husika, hivyo kuongeza tafrani kwa jamii.

3. Umakini

Ripoti ni lazima izingatie maadili na ifanyike kwa umakini kuhusu ukatili dhidi ya wanawake mtandaoni. Mwanahabari anaweza tumia kanuni ya “Usidhuru” ambayo maana yake hakuna madhara kanuni hii ni muhimu itakayosaidia kuepuka au kupunguza madhara.

Mikakati ya kufanikisha kanuni hii, ni pamoja na kuficha utambulisho wa walioathiriwa na ukatili.

Aidha, waweza mlinda muathiriwa kwa kutumia picha zenye ukungu na video potofu, kufanya utafiti wa kina na uthibitishaji wa habari kabla ya kuichapisha ili isiwe taarifa ya muonekano wenye uzushi.

Kuhusu Sheria.

Zipo sheria, miongozo na kanuni zinazoongoza vyombo vya Habari katika kufanya kazi zake, ambazo zinaonesha miiko, kanuni na adhabu, iwapo chombo cha Habari kitakuwa kimevunja sheria kwa kufanya ukatili dhidi ya wanawake mtandaoni.

Sheria hizo, ni pamoja na Sheria ya Huduma za Habari 2016, Sheria ya Maudhui ya Mitandaoni (Online Content Regulation 2020) na Sheria ya Kimakosa ya Mitandao 2015 (Cyber Crime Act), Sura ya 16 kanuni ya Adhabu Sheria Na. 47 ya 1954.

Hivyo, Vyombo vya Habari havina budi kuzingatia sheria hizo katika utoaji wa taarifa kwa jamii, bila kufanya au kushiriki ukatili dhidi ya Wanawake Mtandaoni.

Elimu.

Dar24 Media ilizungumza na baadhi ya Wanahabari tofauti kuhusu mikakati inayotakiwa, ili waweze kuepuka kuwa sehemu ya Ukatili dhidi ya Wanawake mtandaoni, ambao wote kwa pamoja waliomba kuhifadhiwa majina yao.

Kwa nyakati tofauti walisema, “ni muhimu Taasisi za Kiserikali na zisizo za Kiserikali zinazohusiana na mambo ya Habari kuwatafuta Wakufunzi wenye utaalamu na uzoefu kuhusu ukatili dhidi ya Wanawake Mtandaoni wawapatie elimu.”

Wanasema, elimu itasaidia kuzipa kada mbalimbali uelewa juu ya masuala ya kuepuka ukatili wa Wanawake Mtandaoni, kwani wao kama Waandishi baada ya kupatiwa Elimu hiyo wataieneza kupitia nyumba zao za Habari na machapisho binafsi.

Lakini pia, meingine alishauri watumiaji wa mtandao kuwa makini na kuacha kufanya yale yasiyotakiwa katika mtandao ili kujikinga na madhara yatokanayo na matumizi mabaya ya mtandao kwani yatawaletea athari mbeleni.

Aidha, Mwanahabari wa tatu yeye aliigusa Serikali akisema kwamba inapaswa kupitia upya sheria, ili ziweze kuwapa uhakika zaidi wa usalama mtandaoni kwa Wanawake, ili kuweza kushiriki kikamilifu katika TEHAMA ikiwemo majukwaa ya Kidijitali.

Mwanahabari mwingine, alisema yeye binafsi anaona shida ipo katika Vyuo vya uandishi, wengi wa Walimu ni rika moja na Wanafunzi kitu ambacho sio shida bali wanafunzi wanaofanya vizuri kimasomo hubakishwa kuwafundisha wenzao hali ya kuwa hawajaiva kitaaluma maana ualimu una miiko yake, kitu ambacho hupelekea kufundisha kwa nadharia masomo na si maadili na utambuzi wa aina ya makosa ya mara kwa mara mtandaoni.

“Nadhani wahusika Serikali wangepita huku kuna shida vyuoni, lakini pia kuna shida kwenye ajira vyombo vingi vya habari vinatafuta faina hivyo wanachoangalia ni kutafuta watu wenye kiu na Media ambao hata wakiambiwa malipo kidogo wanakubali, hii hupelekea wasio na sifa kuingia kazini na kushindwa kuchuja kipi ni kipi,” aliongeza.

Mmiliki na Mwandishi nguli mmoja naye aliwaangazia Mamlaka ya Mawasiliano Nchini  – TCRA, alisema inatakiwa ichukue hatua stahiki kwa Vyombo vyote vya Habari vinavyofanya ukatili au vinavyochapisha taarifa za ukatili wa mitandaoni.

“Mara nyingi tunashuhudia makosa ya waziwazi kwa baadhi ya Vyombo vya Habari vikichapisha au vikipakia maudhui ya kudhalilisha utu wa Mwanamke, mtoto au Mwanaume, na tunaona kwamba hakuna hatua zozote zinazochukuliwa sasa hii isipokewewa ndipo pale wengine nao wanapoona ni halali kufanya hivyo kiasi inapelekea tatizo kukomaa, japo wanafanya kazi nzuri, lakini TCRA ni lazima wawe macho kila mara,” alifafanua.

Hata hivyo, ifahamike kuwa kwa mujibu wa Kanuni ya 4 ya Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Maudhui ya Mitandaoni), 2018, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania ina jukumu la kutunza kumbukumbu za watoa huduma wote wa maudhui mtandaoni pamoja na kuchukua hatua stahiki za kisheria dhidi ya mtoa huduma yoyote wa maudhui mitandaoni atakayekiuka Kanuni za Maudhui Mitandaoni au sheria nyingine.

TCRA wanasema kamati yake ya maudhui imewahi kuchukua hatua kadhaa ikiwemo kuonya kwa kuviita, kuvifungia ama kuvilipisha faini baadhi ya Vyombo vya Habari kwa kukiuka maudhui ya mtandaoni yanayoshusha hadhi au kuendana kinyume na vifungu vya sheria ya Habari.

Na hii huvikumba Vyombo vile vya Habari ambavyo vimeenda kinyume na Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Maudhui ya Mtandaoni), 2018, ikisomwa pamoja na Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Maudhui ya Redio na Teleuisheni), 2018.

TCRA wanazidi kubainisha kuwa chombo cha habari kinatakiwa kuzingatia weledi na maadili ya uandishi wa habari katika kuweka maudhui mtandaoni na kuhakikisha maudhui yake hayaleti usumbufu au mkanganiko au upotoshaji kwa jamii au mlaji wa maudhui hayo.

Kwa maana hiyo, kwa mujibu wa Kifungu cha 28 (1) (b) na (d) cha Sheria ya Mainlaka ya Mawasiliano Tanzania, Sura ya 172, Marejeo ya Mwaka 2017 TCRA ina meno ya kukukifungia chiombo kinachokiuka maudhui kulingana na kanuni husika.

Aidha, TCRA wanasisitiza kuwa kitendo cha kurusha taarifa isiyo na usahihi na ukamilifu hukiuka Kanuni Na. 7(1)(a) & (b) Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Maudhui ya Mtandaoni), 2018, ikisomwa pamoja na Kanuni Nambal5 (2) (b) (c) ya Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Maudhui ya Redio na Televisheni), 2018.

Hitimisho

DW Akademie imeonesha njia kwa kuanza kutoa mafunzo kwa Vyombo vya Habari, juu ya  namna nzuri ya kuripoti kesi za ukatili dhidi ya Wanawake Mtandaoni.

Elimu hii inahitajika iwe endelevu na ya mara kwa mara, ili waliopata ujuzi waendelee kujiboresha zaidi na kuwa mabalozi wema katika suala la Ukatili dhidi ya Wanawake mtandaoni.

Pia, ipo haja ya Wadau, Taasisi na Mamlaka za Serikali nazo zikapambania suala hili katika utoaji wa elimu sahihi, ili Vyombo vya habari viwe sehemu  kurekebisha na kutoa Habari sahihi na za uhakika, kwani ukatili wa mtandaoni ni jinai.

 

Waziri Mkuu wa zamani aweka mambo hadharani
Wahitimu wapewa mbinu kuepuka matukio ya uhalifu