Ama kweli Duniani kuna mambo! Kuna Watu wapenda sana ushujaa, hawataki kabisa kudharaulika mbele ya jamii na katika hili wapo tayari kufanya lolote kuhakikisha wanalinda heshima zao, ikibibidi hata kwa kufanya hila, kutumia pesa ama kutumia mabavu, ili tu aibuke kifua mbele kwa maslahi binafsi au kutengeneza historia.
Nakumbuka zamani tuliwahi kwenda kucheza Mpira wa miguu katika Shule moja ya Sekondari iliyopo eneo la kambi ya Jeshi huko Mkoani Tabora, tulipofika kwanza tulipokelewa kwa kurushwa kichurachura na Wanajeshi waliokuwa zamu ya ulinzi getini wakidai wanatupa ukakamavu na wanatutoa uraiani.
Baadaye kwa maneno ya upendo walituonesha uwanja kisha kutupatia sharti moja kuwa tutacheza mpira, lakini hakuna kushangilia goli yaani ni kimya kimya nasi tukatikisa vichwa kuashiria tumeelewa.Tulifika uwanjani na kukuta timu pinzani na mpira ukaanza, hadi dakika tisini zinakaribia kutamatika tulikuwa tumewafunga wenyeji wetu 2-0, lakini refa aliitwa na wale Wanajeshi na inadaiwa aliambiwa hakuna kumaliza mpira.
Mpira ukaendelea, lengo lilikuwa ni mpaka pale wenyeji wetu wtakaposawazazisha magoli yote mawili na kibaya walisawazisha kwa hila, halafu wakatengeneza penati ya ‘ajabu ajabu’ tukawa tumefungwa 3-2 na Filimbi ya kumaliza mpira ikapulizwa giza likiwa limetanda. Tuliona ‘poa tu’ kwani moyoni tulikuwa na amani kwamba kiuhalisia sisi ndiyo tulipaswa kuwa washindi.
Hata hivyo, tulidhani yameisha kumbe sivyo kwani tuliitwa na tukaambiwa tukae chini nasi tukatii, hapo mmoja wa wale Wanajeshi akasema, “mpo jeshini mkitoka hapa mtembee mwendo wa ukakamavu mpaka nje ya kambi, halafu mkifika makwenu msilalamike kwamba mmeonewa nadhani wenyewe mmeshuhudia kwamba zimerudishwa goli mbili na likaongezwa la tatu, kiufupi Jeshi huwa halishindwi uwanja wa nyumbani.”
Sikumbuki ilikuwaje ila kwa mbali hisia zinaniambia maongezi ya mtu mmoja mmoja yalianza baada ya kufika mitaa ya Bachu, halafu kila mmoja akawa anajiapiza kamwe hatathubutu kurudi kucheza pale huku kila mmoja akiutafuta mtaa wake, lakini somo tuliloondoka nalo ni kwamba, hakuna kupoteza uwanja wa Nyumbani, nadhani ni kwajili ya kulinda heshima na lilitusaidia.
Nimesimulia kisa hiki, maana nilitaka kukupa kisa kingine ambacho ndicho nilikikusudia kukuletea, ni cha Muitaliano ambaye alikuwa ni Mfalme akiitwa Gaius Caesar Augustus Germanicus (Caligula). Mfamle huyu alijulikana kwa jina la utani kichwa cha moto, siku moja alikuwa akirejea nyumbani akitoka kwenye vita ya uvamizi.
Katika vita hiyo ambayo alitaka kufanya maangamizi dhidi ya Uingereza, Mfalme Caligula alishindwa namna ya kuingia na kufanikisha uvamizi huo kutokana na ulinzi mkali alioukuta, hivyo aligeuka kurudi nyumbani licha ya kuwa na sifa moja kwamba akitamani kitu kitakuwa, sasa akawaza atarudije nyumbani awaambie watu wake ameshindwa vita? heshima itashuka na atadharaulika, itakuwaje?.
Akawaza aibu itakayompata akaona isiwe tabu eti arudi nyumbani mikono mitupu bila uthibitisho wa chochote alichopoka ugenini, akajisemea haiwezekani? hapo Mfalme Caligula aliamua kutangaza vita juu ya kitu chochote cha karibu ambacho angeweza kukutana nacho baharini hata kama iwe ni samaki, lengo apate kulipua mabomu lakini akakosa kuona hata dagaa.
Akafikiria tena kwa kuyatazama mawimbi akaona kama ‘yanamfokea’ yanamletea dharau hapo akasema eti yanajiona kama Mungu wa bahari! hivyo akawaamuru watu wake kuyapiga mawimbi na kukusanya makombora kama uthibitisho wa ushindi na alipofika nyumbani alilakiwa kwa nderemo na vifijo, eti ameshinda vita na amerudi salama bila majeruhi.
Hata hivyo, Wanahistoria hawana uhakika wa asilimia 100 kama hadithi hii ni ya kweli, lakini ukweli ni kwamba watu waliamini kisa hicho cha ‘kubumba’ alichokitengeneza Mfalme Caligula kilikuwa ni cha kweli kumbe ‘Mshua’ alitaka kulinda heshima kwa namna yeyote ile. Watu kama hawa mpaka leo bado wapo, wakitengeneza matatizo na kuyatatua ili waonekane ni watenda miujiza, kumbe wanajivisha kilemba cha ukoka.
Kikubwa tunachotakiwa kufahamu ni kwamba heshima huwa hailazimishwi na hata Wahenga walipata kusema “Atafutaye heshima kwa nguvu, huambulia dharau kwa bei rahisi,” kufosi mambo ni sawa na kujitekenya kisha ukacheka mwenyeaw, hivyo katika maisha ni vizuri kutenda yale yaliyo ndani ya uwezo wako na usiyoyaweza achana nayo haikupunguzii kitu kwani utatengenezea historia iliyojaa ukweli ndani yake, na itakuwa ni funzo jema kwa wengine.