Beki wa Ghana, Daniel Amartey amesema amefikia mwisho wa kuitumikia timu ya taifa ya nchi hiyo maarufu kama Black Stars.
Uamuzi huo ameufikia baada ya kutoka nusu utupu kwenye mchezo baina ya timu hiyo na Msumbiji Uwanja wa Alhassan Ouatarra, Ivory Coast.
Amartey alivua bukta na jezi yake na kuacha nguo ya ndani akionyesha hisia za kukerwa na matokeo hayo.
Iliwalazimu mashabiki wa Ghana kumfunika na bendera ya timu ya taifa kuficha maungo yake.
Beki huyo alisikika akisema: “Nimemalizana na Black Stars, chukueni jezi yenu.”
Amartey alicheza chini ya dakika 10 kwenye mchezo huo wa Kundi B dhidi ya Msumbiji mwanzoni mwa juma hili. Aliwekwa benchi kwenye mechi dhidi ya Cape Verde na Misri.
Amartey alifuta picha zote zinazohusiana na timu ya taifa kwenye akaunti yake ya Instagram.
Ghana walihitaji ushindi kusonga mbele lakini waliruhusu kutoka nyuma kwa mabao 2-0 mpaka sare ya mabao 2-2.