Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amezitaka Kampuni, Taasisi na Watu binafsi wanaotarajia kushiriki Mkutano wa Mining Indaba, kuhakikisha wanaiweka Tanzania katika ramani ya dunia, kwa kutangaza utajiri wa madini na fursa za kiuwekezaji zilizopo.

Waziri Mavunde ameyasema hayo wakati akifungua kikao maalum cha wadau wanaotarajia kushiriki katika mkutano wa Mining Indaba utakaofanyika kuanzia tarehe 5 hadi 8 Februari, 2024 nchini Afrika Kusini.

Amesema kutokana na fursa mbalimbali katika Sekta ya Madini kuanzia kwenye shughuli za utafiti, uchimbaji, utoaji huduma migodini na uongezaji thamani madini ni alama tosha ya kuitambulisha Tanzania kwa sauti moja kwa wadau mbalimbali watakaoshiriki katika mkutano huo mkubwa.

“Kuna baadhi ya nchi duniani wamejikita eneo moja tu la usambazaji wa bidhaa na utoaji huduma migodini. Tunataka watanzania wengi wanufaike kupitia eneo hili na tunapenda kuona uzalishaji wa bidhaa mbalimbali zinazohitajika migodini zizalishwe zinafanyika hapa nchini,’’ alisema Mavunde.

Aidha, amesema bado Sekta ya Madini nchini haijatoa mchango unaostahili kiuchumi ikilinganishwa na utajiri wa rasilimali madini pamoja na fursa zilizopo na kusisitiza kuhusu shughuli za utoaji huduma na usambazaji wa bidhaa migodini kuwa ni eneo ambalo kama Wizara inalichukua kwa uzito kutokana na manufaa yake na kwamba ni miongoni mwa maeneo ambayo imeyapa kipaumbele katika mkutano huo.

Kuhusu suala la utafiti, Waziri Mavunde amesema ni eneo ambalo Tanzania inatarajia kulitangaza kupitia mkutano huo lengo likiwa ni kuvutia uwekezaji katika shughuli za utafiti wa madini na hususan madini mkakati ambayo ndiyo mwelekeo wa dunia kwa sasa kutumia madini muhimu na mkakati kuzalishaji nishati safi.

Naye, Mwenyekiti wa Chemba ya Migodi Tanzania, Mhandisi Philbert Rweyemamu akizungumza katika kikao hicho amewataka wote watakaoshiriki kuitendea haki Tanzania kwa kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika mkutano huoili kutoka na matokeo chanya huku akiainisha shughuli mbalimbali ambazo Tanzania inatarajia kushiriki wakati wa mkutano huo ikiwemo kuwa na siku maalum ya kuinadi Tanzania katika mkutano adhimu wa Mining Indaba.

Akizungumza katika kikao hicho, Katibu Mkuu Wizara ya Madini Kheri Mahimbali amesema kikao hicho ni nyenzo muhimu katika utekelezaji wa Sera ya Madini ya Mwaka 2009 ya kuvutia uwekezaji katika Sekta ya Madini ambapo mkutano wa Mining Indaba ni moja ya mikutano ambayo wizara inategemea kuitumia kuendelea kuvutia uwekezaji.

Wavuvi haravu wakumbushwa nguvu ya Dola
Daniel Amartey aikataa Black Stars