Shirikisho la Soka Algeria ‘FAF’, limemfuta kazi Kocha wa timu ya taifa, Djamel Belmadi kufuatia kushindwa kufanya vizuri katika michuano ya Kombe la Mataifa Afrika (AFCON), inayoendelea nchini Ivory Coast.
Uamuzihuo umekuja baada ya timu hiyo kupoteza bao 1-0 dhidi ya Mauritania katika mchezo wa mwisho hatua ya makundi, uliochezwa juzi Jumatano (Januari 24) Uwanja wa Bouake.
Ushindi wa Mauritania uliifanya Algeria kuondoshwa katika michuano hiyo msimu huu.
Maamuzi hayo ya ‘FAF’ yanasitisha mkataba wa Kocha Belmadi ambao ulitarajiwa kumalizika mwaka 2026 baada ya kufikia makubaliano pande zote mbili.
Rais wa ‘FAF’ Walid Sadi ametangaza kwamba wameachana na Kocha Belmadi kufuatia timu yao kuondolewa hatua ya makundi msimu huu.
“Tumefikia makubaliano pande zote mbili na kuamua kuachana na Kocha Belmadi kufuatia kushindwa kufanya vizuri katika michuano ya AFCON msimu huu.
Tunamshukuru kwa mudawake kwetu, hivyo tunamtakia kila la kheri huko atakapokwenda kutafuta changamoto nyingine,” amesema Rais Sadi.
Katika michuano ya msimu huu, Algeria ilipata sare ya bao 1-1 dhidi ya Angola, baadae ilitoa sare nyingine mbele ya Burkina Faso kabla ya kufungwa bao 1-0 na Mauritania.
Hii inakuwa mara ya kwanza wa Algeria kutolewa katika michuano hiyo hatua ya makundi tangu mwaka 1994.
Belmadi alianza kuinoa Algeria mwaka 2018, ambapo aliisaidia timu hiyo kubeba taji la AFCON mwaka 2019 nchini Misri.