Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imeishauri serikali kuutumia Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kuainisha viwango vya usalama na afya katika samani na vifaa mbali mbali vya ofisi kabla ya manunuzi kufanyika ili kuepuka kununua samani na vifaa visivyokidhi viwango stahiki.
Ushauri huo, umetolewa mara baada ya Kamati hiyo kupatiwa semina ya masuala ya Usalama na Afya mahali pa kazi iliyotolewa na wataalam wa OSHA wakiongozwa na Mtendaji Mkuu, Khadija Mwenda.
Mwenyekiti wa PAC, Naghenjwa Kaboyoka, amesema kupitia semina hiyo, wameweza kubaini kuwa samani na vifaa mbali mbali visivyozingatia viwango vya usalama na afya vimeendelea kununuliwa katika majengo na ofisi za serikali licha ya kuwepo kwa Taasisi ya OSHA ambayo ingeweza kutoa ushauri juu ya viwango stahiki.
Aidha, Mwenyekiti huyo ameeleza kuwa OSHA inapaswa kushirikishwa kikamilifu katika miradi ya ujenzi wa majengo ya serikali hususan katika Mji wa Serikali unaoendelea kujengwa katika eneo la Mtumba Jijini Dodoma ili ujenzi huo uweze kuzingatia uwepo wa miundombinu rafiki kwa ajili ya kulinda afya na usalama wa watumishi wa umma na wananchi kwa ujumla.
“Tumeishauri Taasisi yetu ya OSHA kwenda kwenye Taasisi zote za serikali na mashirika ya umma kuwaeleza kuhusiana na umuhimu wa kununua samani na vifaa vinavyozingatia afya na usalama kwa wafanyakazi ili kuepuka hasara inayoweza kusababishwa na ununuzi wa samani na vifaa visivyokidhi viwango stahiki katika kulinda afya na usalama wa watumiaji wake.” alisema.
Kwa upande wake, Mjumbe Venant Protas, ameipongeza OSHA kwa maboresho ambayo wameendelea kuyafanya katika utendaji wake na kuongeza kuwa, “mwaka jana OSHA walifika mbele ya Kamati yetu na tukawashauri kufanya maboresho kadhaa ambayo wameyafanyia kazi. Miongoni mwa mambo waliyoyaboresha ni kujiunganisha na kuwa na mawasiliano mazuri na Taasisi nyingine za umma”, amesema Protas
Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, amesema Taasisi yake ipo katika nafasi nzuri ya kutekeleza ushauri uliotolewa na Kamati kutokana na serikali kuridhia kujumuishwa kwa masuala ya usalama na afya katika kanuni za utumishi wa umma na kuandaa miongozi ya utekelezaji wake.