Tanzania, imechaguliwa kuwa moja ya nchi nane za Afrika zitakazopewa kipaumbele na Italia kupitia mpango mpya wa kimkakati wa Mattei (Mattei Plan), ambapo kiasi cha Euro bilioni 5 za awali kimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo ya kipaumbele kupitia Mpango mpya wa Kimkakati uliopo katika sekta ya nishati, elimu na kilimo.

Taarifa hiyo imetolewa na Rais wa Chama cha Wafanyabiashara wa Italia, Mhandisi Alfredo Cestari alipokutana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba pembezoni mwa Mkutano wa Nne, wa Wakuu wa Nchi za Afrika na Italia unaoendelea jijini Roma, Italia.

Amesema, utekelezaji wa mpango huo utaanza mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa Wakuu wa nchi za Afrika na Italia, ambapo Serikali ya nchi hiyo itafadhili miradi ya kipaumbele kwa nchi nane za awali za Afrika. Hatua hiyo itahusisha pia kugharamia gharama za upembuzi yakinifu ya miradi itakayopendekezwa.

Katika hatua ya utekelezaji ya mpango huo, ujumbe wa wataalam kutoka Chemba ya Biashara ya Italia ikiongozwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia, Dkt. Edmondo Cirielli unatarajiwa kuwasili nchini Tanzania ndani ya mwezi mmoja kwa ajili ya kukutana na timu ya wataalam ya upande wa Tanzania kwa ajili ya kukamilisha hatua za awali za utiaji saini wa ushirikiano huo wa pande mbili utakaohusisha utekelezaji wa miradi itakayopitishwa na pande mbili.

Kwa Upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba ameipongeza Serikali ya Italia kwa kuonesha nia ya kuimarisha uhusiano wake na nchi za Afrika kupitia Mpango mpya wa Kimkakati wa Mattei (Mattei plan) ambapo sekta ya nishati, elimu na kilimo zimepewa kipaumbele.

Pamoja na mambo mengine, mkutano huo umelenga kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji, ili kuongeza kiwango cha biashara na uwekezaji baina ya mataifa hayo mawili kupitia mpango mpya wa Mattei, (Mattei Plan).

Azam FC wamedhamiria 2023/24
Jacinto Dala: Tulistahili Robo Fainali