Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia Mabaraza ya Ardhi na Nyumba imeshiriki uzinduzi wa Wiki ya Sheria jijini Dodoma yakiongozwa na Spika wa Bunge la Tanzania, Dkt. Tulia Ackson uliofanyika katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma ukitanguliwa na matembezi ya uzinduzi wa Wiki ya Sheria.

Akizungumzia ushiriki wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba, Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi Dodoma, Jackson Kanyerinyeri amesema kuwa moja ya jukumu lao ni kutoa elimu kwa wananchi wanaotembelea banda hilo katika masuala ya ardhi, migogoro ya ardhi namna inavyotatuliwa katika mabaraza hayo hadi kutolewa hukumu.

Amesema, wamepata wasaa mujarabu wa kuwaeleza wananchi juu ya mabadiliko ya Sheria Na 3 ya 2021 ambayo imeondoa mamlaka ya mabaraza ya Kata kusikiliza kesi za migogoro ya ardhi badala yake mabaraza hayo yana jukumu la kusikiliza na kusuluhisha migogoro baina ya wananchi ikishindikana migogoro hiyo iwasilishwe Baraza la Ardhi na nyumba la wilaya na kupewa cheti ndani ya siku 30.

Aidha, Kanyerinyeri ameongeza kuwa wanaendelea kuwasistiza wananchi wamalize migogoro ya ardhi kwa nyia ya mazungumzo na mapatano hatua inayookoa muda, kuondoa uhasama na inawapa wananchi muda wa kufanya shughuli za maendeleo na kuinua uchumi wa familia na taifa kwa ujumla.

Wiki ya Sheria 2024 imeanza Januari 24 na inatarajiwa kuhitimishwa Januari 30 yakiongozwa na kaulimbiu “Umuhimu wa Dhana ya Haki kwa Ustawi wa Taifa: Nafasi ya Mahakama na wadau katika kuboresha Mfumo Jumuishi wa Haki Jinai.”

Mbinu za uhalifu zazidi kugonga mwamba
Benchikha: Tupo tayari kumkabili Tembo