Na Humphrey Edward.

Wengi wetu tunatambua na kuelewa kuwa Uongozi ni mamlaka au karama ya kuwaonyesha watu njia kwa vitendo, ambapo mtu yeyote ambaye ni Kiongozi yeye hupimwa kwa jinsi ambavyo anaweza kuleta ushawishi kwa watu na kuyafikia maendeleo yaliyotarajiwa.

Kiongozi bora huwa hana muda wa kulalamika, bali hutafuta ufumbuzi wa matatizo ya Wananchi au watu walio chini yake na ieleweke kuwa Kiongozi wa kweli akiongea, watu husikiliza, kama ambavyo malengo makubwa katika uongozi wa Mwalimu Nyerere yalivyojumuisha kauli mbiu ya siasa za kutokufungamana na upande wowote, kujenga ujamaa na kujitegemea.

Watu wengi humkumbuka Baba wa Taifa na Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwl. Julius Kambarage Nyerere kwa mambo mengi mazuri aliyoyafanya, ikiwemo kuacha umoja, mshikamano na amani, lakini kubwa zaidi ni uwajibikaji wake wenye uadilifu na hotuba zake ambazo zilisheheni maneno yenye hekima na mguso kwa jamii.

Yapo mambo ambayo hayatasahaulika kumuhusu Hayati Mwalimu Nyerere ikiwemo usisitizaji wake wa maadili akisema mtu akiwa Kiongozi basi atatakiwa awe na kitu cha ziada na ndiyo maana alikuwa akisema Kiongozi ni sharti ajiheshimu na kama ni uhuni basi akaufanyie barabarani huku akisisitiza kuwa ni muhimu kutatua kero na matatizo ya Wananchi.

Baba wa Taifa, Mwl. Julius Kambarage Nyerere.

Moja kati ya nukuu zake wakati wa utatuzi wa changamoto mbalimbali Nchini aliwahi kusema kwamba, “hatuwezi kuwa na matumaini ya kutatua matatizo yetu kwa kujifanya kuwa hayapo,” akimaanisha ni lazima kufikiria juu ya changamoto tulizonazo badala ya kuyafunika kwa kudhani yameisha kwani hata Wahenga walipata kusema mficha maradhi, mauti humuumbua.

Mwalimu alituasa kuwa, unapokuwa Kiongozi hakikisha pia unajenga tabia ya kujisomea, ili kila uchwao upate maarifa na taarifa mpya ikiwezekana kabla ya Watu unaowaongoza, akiishi katika dhana yake ya kupenda umoja, kuwa na upendo, mshikamano, amani na haki kwa Watanzania na Waafrika kiujumla.

Aidha, aliasa kila siku kuwa Kiongozi lazima apime kila anachotaka kuzungumza kwa umma maana maneno ya Kiongozi siku zote ni nukuu na ndiyo maana tunaona mpaka leo, watu wengi bado wananukuu Maneno ya Mwalimu Nyerere ambaye alisimamia sera za kujali utu na ubinadamu.

Lakini jambo hili, kwa siku hizi ni tofauti kwani tunashuhudia Kiongozi akiongea ndivyo sivyo mbele ya kadamnasi, yaani badala ya kufundisha, kuonesha njia, kuwa mfariji na hata kuwaweka Watu pamoja, yeye anageuka kuwa mfitini, kinara wa kukashifu, kinara wa Propaganda, mpenda sifa au kusifia alichokifanya nk.

Waweza isikiliza hotuba ya Kiongozi kuanzia mwanzo mpaka mwisho usisikie mipango thabiti ya kuwainua watu kiuchumi, kutatua kero, kuona fursa na kuzitafutia njia itakayoleta matokeo chanya, bali utasikia anashambulia watu, anasifia watu, anatumia maneno ambayo hata mtu ambaye siyo Kiongozi anabaki na maswali kama anayezungumza pahala hapo ni Kiongozi kweli.

Hili linatafakarisha, kiasi hupelekea maswali ya kina je, hiki anachozungumza Kiongozi wangu kinaweza tumika kama nukuu kwa vizazi vijavyo? ni kwanini baadhi ya Viongozi hawachagui maneno, hawafundishi, hawaunganishi watu, hawaheshimu Katiba, Sheria, Kanuni, taratibu na tamaduni zetu, ni kwanini hawana maono ambayo yatasaidia kusogeza mbele gurudumu la ujenzi wa Taifa?

Na ndio maana pia kuna maneno ambayo Mwalimu Nyerere aliyewahi kuyasema nanukuu, “itakuwa yote ni makosa na si jambo la muhimu kuhisi kuwa lazima tusubiri hadi Viongozi wafe ndio tuanze kuwakosoa,” inatafakarisha sana na kwa majira ya sasa ni kinyume kwani waweza kuwa unakosea na watu wanakupigia makofi, lakini ukikosekana manung’uniko huanza na ukifa wataongea mengi zaidi.

Kuna haja ya Wazee wetu kutujibu nini jawabu la mambo haya na ndio maana nilimtembelea Mzee Philip Mangula nyumbani kwake jijini Dodoma, yeye ni mmoja kati ya Viongozi wakongwe na wenye historia ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na katika majibu yake hakuwa mbali na kauli ya Mwalimu Nyerere, kwani aliwataka Vijana kupenda kujisomea na kujibidiisha katika safari zao kisiasa.

Baba wa Taifa, Mwl. Julius Kambarage Nyerere.

Anasema, “hili la Mwalimu yeye alikuwa anaamini katika misingi ya uongozi, alipenda watu wake. Na kuhusu uongozi kiujumla unahitaji kujituma na kujitolea, ni wito wa kuijua siasa na si kujua kuongoza kwani kuongoza watu ni karama na hivyo ni vyema kuandaa misingi kuanzia ngazi ya shina.”

Mzee Mangula anasisitiza kuwa kwasasa dunia imekuwa ni kijiji lakini hiyo haifanyi mtu ashindwe kujibidiisha katika utafutaji wa maarifa, hivyo ni vyema wakajiwekea utaratibu ambao utakuja kuwafaa katika maisha yao ya baadaye, kitu ambacho waweza kukubaliana nacho kwani ukiwa na maarifa mengi hutaongea mambo kwa wakati uliopo, bali utangalia kesho yako na ile ya wanaokuzunguka.

Anasema, “ili ufanikiwe tenga muda wa kutosha kuishughulisha akili na nafsi yako kuyafikiria na kuyachakata mambo yako kwa utulivu, kwasababu huko ndiko kwenye vyanzo vyote vya nguvu za hatua zako katika kuielekea hatma yako, lakini haya yote uyafanye huku ukiwa na fikra kwamba mafanikio pacha wake ni changamoto, zipo changamoto.”

Philip Japhet Mangula ni kiongozi wa enzi za uongozi wa kofia mbili ambaye aliwahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera (1993-1996), na wakati huohuo akiwa ni Katibu wa Chama cha Mapinduzi – CCM, Mkoa akiwa na historia ndefu ndani ya CCM na siasa kiujumla, Mwandishi wa habari, kada na kiongozi wa CCM kwa ngazi mbalimbali ikiwemo ile aliyoistaafu kwa hiari 2023, ya Umakamu Mwenyekiti wa CCM – Bara.

Mzee Philip Mangula.

Aidha, katika kutaka kufahamu zaidi, pia nilizungumza na Mbunge wa Iringa Mjini (CCM), Jesca Msambatavangu, yeye alisema matendo ya baadhi ya viongozi wa sasa ni kama yamekosa dhana ya kitaaluma inayompa mhusika madaraka na uwezo wa kuwawezesha wale wanaongozwa naye kuunganisha nguvu, stadi na vipaji vyao na kuvitumia, ili kufikia malengo yao.

Anasema, “kuongoza ni kujua lengo la wale wanaoongozwa na njia ya kufikia lengo lao, Serikali inatakiwa kuendelea kudumisha na kuimarisha maadili ya Kitanzania kwa mustakabali wa vizazi vijavyo. Taifa liwekeze kwa mustakabali wa vizazi vijavyo, unahitajika umakini pasi na kukopa mila na desturi za mataifa ya nje ambayo yapo kinyume na maadili ya Kitanzania na hapo tutafaulu.”

“Na ndio maana sasa baadhi ya Viongozi wamekuwa wanashindwa kuibana Serikali katika mambo ya msingi kwa kuhofia kupoteza nafasi zao, huku wakisahau kwamba kitendo cha kusifia kila kitu na ukimya wao unawaumiza Wananchi, waache unafiki. Maendeleo yoyote huja kwa ushirikiano ni lazima awepo kiongozi ambaye atawakilisha wengine, wanapoaminiwa na kushindwa kuzitumia nafasi hizo kiufasaha wanasababisha adha kwa waliowaamini,” alisisitiza Msambatavangu.

Alimaliza kwa kudai kuwa, “Kiongozi yeyote anayetambua majukumu yake huwa ni mfuatiliaji wa mambo na hutoa kauli zinazotosha kukupa picha ya moja kwa moja ya wapi mnaelekea katika utekelezaji wa mambo au shughuli za kijamii, kiuchumi na kimaendeleo huku akipewa wadhifa wa ubeba maono na kujivunia uwepo wake, hili la sifa na hata kukosa weledi ni wazi kuwa lina mapungufu.”

Mbunge wa Iringa Mjini (CCM), Jesca Msambatavangu.

Wahenga walipata kusema ‘Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo’ lakini pia wakaongeza ‘Samaki mkunje angali mbichi’ haitoshi wakaongeza tena jingine ‘mdharau mwiba mguu huota tende’ wakatoa na nyongeza kwamba ‘usipoziba ufa utajenga ukuta,’ lengo lao kuu lilikuwa ni kuhakikisha kwamba uimara wa jambo lolote huwa na msingi imara kuanzia ngazi ya chini.

Aliyekuwa Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa naye akawa na maoni kuhusu hili akisisitiza kujenga mazoe ya kusoma vitabu, ili kujiongezea maarifa huku akitumia msemo wa Mwandishi na mhamasishaji Rick Warren kuwa “the moment you stop learning, you stop leading.” akimaanisha ukiacha kusoma unaacha kuongoza.

Kama ilivyo kwa wahojiwa wa awali, Msigwa naye aliyasema haya wakati akifanya mahojiano nami nilipomtembelea nyumbani kwake Kihesa mjini Iringa na akaongeza kwamba maarifa ya mtu huongezeka kwa kusoma vitabu mbalimbali vyenye ubora na maarifa vinavyoweza kumsaidia mtu kupiga hatua.

Anasema, “Kama kuna mtu amefanikiwa zaidi yako, kwenye eneo lolote la maisha, kuna vitu anajua ambavyo wewe hujui badala ya kumwonea wivu au kumwogopa, mwombe akushirikishe ni aina gani ya vitabu anasoma, hapo utapata vya kuanzia. Uongozi unahitaji weledi na maarifa mapya.”

Peter Simon Msigwa ni Mwanasiasa maarufu nchini na aliwahi kuwa mbunge wa Iringa Mjini kwa vipindi viwili kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ambaye kwasasa anaendelea na shughuli za kisiasa huku akijihusisha na Kilimo.

Peter Simon Msigwa.

Hata hivyo kuna ujumbe muhimu hapa, “sababu mojawapo inayowasumbua Baadhi ya Viongozi wengi wa nyakati hizi kuyafikia malengo yao ni pamoja na kutothamini kile kidogo kinachoweza kupatikana kwa wakati sahihi na uliopo, huku wakitamani kikubwa ambacho hawajui watakipata lini na kubaki wakisifia jambo hata kama ni baya ili waonekane na wakubwa zao, hiyo ni mbaya inatuumiza sisi wa chini,” ilikuwa ni sauti ya Mwananchi Julius Bega akiongelea uhalisia wa baadhi ya Viongozi wasiotambua maana ya Uongozi.

Uongozi wenye weledi hutambua pande mbili za shilingi kwamba kuna kusifiwa na kukosolewa, lakini pia kuongea vitu vyenye uhalisia na vinavyogusa maisha ya watu ama kuacha alama ya ujumla katika jamii na hata kukosoa baadhi ya mambo ambayo hayapo sawa, kwani hata wakati wa uongozi wa Mwalimu Nyerere hakukosoa tu watu wake lakini uligusa hadi nchi tajiri za ulimwengu, mfano mwaka wa 1968 alihoji sheria za Shirika la Umoja wa Afrika (OAU) kwa kutumia sera za Biafra kutoka Nigeria.

Aidha, baadaye mwaka 1975 aliushambulia Umoja wa Muungano wa Afrika (OAU) kwa sababu ilipanga kufanya mkutano wake mkuu nchini Uganda, ambapo Rais Idi Amin alikuwa akiwatendea watu wake ukatili wa kila aina. na ikumbukwe kuzorota kwa mahusiano ya Tanzania na nchi za Uganda na Kenya kulichangia kuanguka kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mnamo 1977, ambayo ilikuwa imeanzishwa miaka 10 kabla kwa malengo ya kukuza maendeleo ya kiuchumi kati ya nchi hizo tatu.

Jawadu Mohamed.

Hivyo, baadhi ya Viongozi wetu kuendelea kutumia muda wa Wananchi wanaowasikiliza kwa kusema mambo ambayo hayana mashiko, kutokuzungumzia sera, mipango yao ya baadaye na hata kutoa kauli za matumaini kwa magumu yanayoikabili jamii ni sawasawa na kuwakosea, yafaa kuitafuta heshima kwa mema watakayoyatenda kwa umma na si kusifia visivyo na sifa au kuongea mambo kwa kuangalia maslahi binafsi.

Uongozi ni dhamana na ndiyo maana hata baadhi ya watu walioshiriki kufanikisha Makala hii, akiwemo Mchambuzi wa mambo ya kisisasa, Jawadu Mohamed anasisitiza kusimamia haki na kuwa na uongozi wenye kuacha alama kwa jamii na si machungu ambayo yataumiza vizazi na vizazi pale watakapokuwa wakisimulia matukio yaliyopita, hivyo upo umuhimu wa Viongozi wetu wakabadilika na kurudi katika mstari na kutumikia viapo vyao kwa uadilifu huku wakiongeza maarifa mapya yatakayowasaidia kuacha alama.

Ikumbukwe kuwa ni vigumu kusonga mbele, ikiwa umeziacha nyuma fikra zako, maana mambo yote yaliyopita yatabaki kuwa historia na hakuna jinsi au namna yoyote unayoweza kuifanya, ili kuibadili historia. Lakini kupitia sasa Viongozi wetu bado wana nafasi na fursa nzuri ya kuitengeneza kesho kwa ajili ya Taifa la Watanzania na wakaacha funzo lenye misingi kwa umma siku zote, kwani UKIPANDA HEKIMA UTAVUNA HESHIMA.

Sopu, Akaminko watajwa Simba SC
Guede amchimba mkwara mzito Inonga