Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amezielekeza Ofisi ya Rais–TAMISEMI na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia zihakikishe Wanafunzi wote wenye rika legwa wanaandikishwa shuleni kwa wakati, ziendelee kusimamia udhibiti wa michango holela shuleni pamoja na kuhakikisha fedha zinazotengwa kwa ajili ya mafunzo ya utekelezaji wa mtaala mpya na kuzitumia kama ilivyokusudiwa.
Majaliwa ametoa maagizo hayo hii leo Februari Mosi, 2024 Bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha Taarifa kuhusu utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo 2014, Toleo la 2023 na Mitaala ya Elimu ngazi ya Elimu Awali, Msingi, Sekondari na Elimu ya Ualimu katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu.
Mbali na maelekezo hayo, pia ametoa wito kwa Watanzania kuhakikisha wanafunzi wote wenye umri wa kujiunga na elimu ya awali, darasa la kwanza na kidato cha kwanza wanadahiliwa na kuanza masomo mara moja.
“Ninatoa rai kwa viongozi wote kuendelea kuwasimamia walimu kwa upendo na uadilifu ili kuwatia moyo na kuongeza ari ya uwajibikaji na kuleta matokeo chanya ya ufundishaji na ujifunzaji,” alisema.