Gazeti la DAILY POST la nchini Nigeria limeripoti kuwa Nahodha na Mshambuliaji wa Kikosi cha Super Eagles Ahmed Musa na Beki wa Kulia Bright Osayi-Samuel wataukosa mchezo wa Robo Fainali wa ‘AFCON 2023’ dhidi ya Angola.

Nigeria iliyotinga hatua ya Robo Fainali kwa kuichapa Cameroon katika mchezo wa Hatua ya 16 Bora itaikabili Angola iliyoing’oa Namibia, kesho Ijumaa (Februari 02) katika Uwanja wa Felix Houphouet Boigny mjini Abidjan.

Gazeti la DAILY POST limeripoti kuwa Musa alikumbwa na majeraha ya Paja akiwa katika mazoezi ya kujiandaa na mchezo huo, huku Osayi-Samuel akiendelea kuwa chini ya uangalizi kufuatia maumivu ya goti yanayomkabili kwa sasa.

Hadi sasa Musa hajapata nafasi ya kuwa sehemu ya kikosi cha Nigeria tangu Fainali za Afrika ‘AFCON 2023’ zilipoanza Mwezi Januari, lakini hatua ya kuumia akiwa mazoezini inaendelea kumfanya kukosekana kabisa katika kikosi ambacho kinatarajiwa kuikabili Angola.

Kwa upande wa Osayi-Samuel ameshacheza michezo miwili ya ‘AFCON 2023’.

Kikosi cha Nigeria kinatarajiwa kufanya mazoezi yake ya mwisho leo Alhamis (Februari 01) katika chuo cha Polisi Cocody, mjini Abidjan, tayari kwa kukabili Angola ‘Palancas Negras’.

Maagizo ya Waziri Mkuu kwa TAMISEMI, Wizara ya Elimu
MALIMWENGU: Wafanya sherehe kumtisha Shetani