Kocha Mkuu wa Geita Gold FC, Denis Kitambi, amesema Usajili wa Dirisha Dogo uliofanywa na Simba SC utaufanya mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaowakutanisha Februari 12, mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini, Mwanza kuwa mgumu kwao.

Akizungumza mjini Morogoro ambako wameweka kambi, Kitambi, amesema maingizo mapya katika kikosi cha Simba SC yamewachanganya, hasa kwenye benchi la ufundi.

“Tulijua tutacheza dhidi ya Simba SC, kikubwa ni sisi tunahitaji pointi tatu kwa sababu tunacheza tukiwa nyumbani, lakini changamoto ninayoiona kuelekea katika mchezo huo ni mpinzani amefanya usajili mpya, kwa hiyo inabidi uangalie hayo maingizo mapya wana ubora gani, wanachezaje kitu ambacho hatuwezi kufahamu kwa sasa, tunakwenda kucheza na baadhi ya wachezaji ambao hatuwafahamu vyema,” amesema Kitambi.

Kocha huyo amesema kitu pekee anachotegemea ni mechi tatu (Mashujaa FC, Tabora United na Azam FC) kabla ya kucheza na Simba watazitumia kujiimarisha na kuongeza mbinu.

Katika dirisha dogo la usajili, Simba SC imewaongeza Boubacar Sarr, Salehe Karabaka, Omar Jobe, Freddy Michael, Ladack Chasambi na Edwin Balua.

Majaribio uzalishaji Bwawa la Nyerere yanaendelea
Ajali ya moto: Waliotoa kibali ni watepetevu - Ruto