Heldina Mwingira
Kama inavyotambulika, sheria ni mfumo wa kanuni na taratibu zilizowekwa kwenye jamii na mamlaka kwa ajili ya kuwaongoza matendo yao na mahusiano yao. Nchi yeyote huwa na sheria ambazo hutoa miongozo, kanuni, adhabu na namna gani ya kuishi kwa amani na upendo katika nchi husika. Nchini Tanzania zipo sheria zilizowekwa kwenye jamii na mamlaka kwa ajili ya kuwaongoza jamii husika. Kutokana na ukuaji wa teknolojia ikabidi zitungwe sheria zinazolinda na kuzuia ukatili mitandaoni kama ifuatavyo.
Sheria ya Maudhui ya Mitandaoni (Online Content Regulation 2020) ambayo inakataza na kutoa adhabu kurusha maudhui ya udhalilishaji ikiwamo picha/video za utupu, lugha za udhalilishaji zinazokwenda kinyume na utamaduni wa Mtanzania.
Sheria ya Kimakosa ya Mitandao 2015 (Cyber Crime Act) ambayo kinakataza na kupinga uonevu mtandaoni kuwa ni kosa kisharia kwa mtu yoyote kufanya uonevu wa aina yoyote kwa kutumia njia za kieleketroniki na kufanya hivyo ni kosa kisharia, a yeyote atakayekutwa na kosa hili atatumikia kifungo, kisichozidi miaka 3 jela au zaidi, au kulipa faini isyopungua milioni tano au vyote kwa pamoja.
Ijapokuwa kuna uwepo wa sheria hizo, lakini bado ukatili mtandaoni unashamiri hasa ukatili dhidi ya Wanawake mtandaoni, hii imeoneshwa katika ripoti ya baraza la haki za binadamu ambayo inasema kuna hatari kubwa kwamba matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (ICT) bila ulinzi sahihi unaozingatia haki za binadamu inaweza ikawa sababu ya kupanua wigo na kuongezeka kwa ukatili dhidi ya wanawake mtandaoni.
Kutokana na mapinduzi ya kidijitali, hii imeonekana kuwa hii ni aina nyingine ya ukatili unaoshamiri na unaowezeshwa na mtandao dhidi ya Wanawake, ikitokana na kuongezeka kwa watu wanaotumia mitandao kama ilivyooneshwa kwenye takwimu zilizotolewa Oktoba, 2023 na wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, kuwa matumizi ya TEHAMA yameongezeka kutoka watumiaji milioni 29.9 kwa mwezi Aprili 2022 hadi kufikia watu milioni 34.04 kwa mwezi Juni 2023.
Inapaswa kukumbuka aina yoyote ya ukatili ni kinyume cha sheria. Uwepo wa Sheria kuhusu ukatili mtandaoni husaidia watu walioathiriwa na ukatili mahsusi wanawake na katika hili Dar24 Media kwa kutaka kujua sheria inazungumzia vipi ukatili dhidi ya Wanawake mtandaoni ilimtafuta mwanasheria George Ngwembe.
Alisema, ‘zipo sheria mbalimbali ambazo zinakataza kuwadhihaki na kuwadhalilisha watu kwa kuchapisha picha au video ambazo hazina staha mtandaoni, sheria hizo zinatoa muongozo jinsi ya kuwajibika ikitokea mtu amevunja, japokuwa waathiriwa wengi wa ukatili mtandaoni ni jinsia ya kike lakini hamna sheria mahsusi kwa wanawake tu, katika nchi yetu ziko sheria jumuishi.”
Kuhusu uwepo wa kesi kama hizo katika vyombo vya dola akajibu kesi kama hizo ni mara chache kuripotiwa ijapokuwa kuna wimbi kubwa la ukatili wa mtandaoni Ngwebe anasema, ‘Mimi binafsi sijawahi kupata kesi kama hii ijapokuwa waathirika wa ukatili wapo na kesi namna hizi ni za jinai na asilimia kubwa waaathirika wa ukatili huu hupata madhara lakini hupuuzia na hawaendi mahakamani.”
Tulitaka pia kufahamu sababu zinazoweza kupelekea watu wengi kutoripoti kesi ijapokuwa wametendewa ukatili mtandaoni, ambapo Mwanasheri Ngwembe hakusita kutoa majibu.
Alisema, ‘mara nyingi watu hawaendi kuripoti kokote kwa sababu mbalimbali kama vile kuona wanapoteza muda mwingi, kwa kwenda polisi na kisha kuzungushwa na kufika mahakamani atoe ushahidi na wakati mwingine kushindwa kuendelea na shughuli nyingine za kiuchumi kwa kuzingatia tarehe ijayo aliyopangiwa pia kuogopa kuingia gharama mbalimbali kama vile nauli na gharama nyinginezo ili kesi iendelee kuunguruma.”
Hata hivyo alibainisha kuwa, “baadhi ya wanawake walioathirika wakishauriwa wakaripoti huwa hawataki kwa sababu wanaona kupitia ukatili waliofanyiwa wamepata umaarufu kwenye mtandao,hivyo wanaona sawa hata kama wamedhalilishwa japo haipaswai kuwa hivyo.”
“Wanawake walioathirika na ukatili mtandaoni inawapasa watafute haki zao kisheria. inapaswa kwenda polisi kuandaa majalada, kufanya uchunguzi wakimaliza kufanya uchunguzi waende ofisi ya taifa ya mashtaka na kisha mahakamani na kupata adhabu stahiki kulingana na sheria kwa wafanya ukatili, hii itasaidia kupunguza kama sio kumaliza kabisa changamoto hii ya ukatili dhidi ya wanawake mtandaoni,” alisisitiza.
Umefika wakati jamii ibadilike na kulichukulia suala hii la ukatili dhidi ya wanawake mtandaoni kwa uzito. Kama tafiti zinavyoonesha, Wanawake ni waathirika wakubwa wa ukatili wa mtandaoni ukilinganisha na wanaume.
Hivyo zinahitajika juhudi kubwa kutoka asasi za kiraia, Jeshi la Polisi wadau wa sharia, taasisi binafsi na Serikali katika kuwaelimisha kuwapa uelewa jamii kuhusu sheria na adhabu atakazopata iwapo atavunja sharia.
Lakini vilevile uwekwe utaratibu wa kuwasaidia Wanawake kupata haki zao endapo itathibitika kuwa mwanamke amefanyiwa ukatili mtandaoni basi mtenda apewe ahabu kulingana na utaratibu wa sharia unavyoelekeza, ili kusaidia kupunguza na kuondosha kabisa mambo kama hayo.