Kiungo Mshambuliaji wa Arsenal, Bukayo Saka, ambaye ana asili ya Nigeria juzi aliishangilia timu hiyo baada ya kutinga fainali ya Kombe la Mataifa Afrika ‘AFCON 2023’, ilipoitoa mashindanoni Afrika Kusini.
Saka ana asili ya Nigeria lakini amekuwa akiitumikia timu ya Taifa ya England, ila juzi alifurahishwa na taifa hilo kutinga fainali ilipopata ushindi wa Penati 4-2, baada ya sare ya bao 1-1 ndani ya dakika 120 za mchezo.
Hii ilikuwa mara ya kwanza Nigeria inakwenda Fainali ya Kombe la Mataifa Afrika baada ya kupita miaka 11 na sasa itavaana na wenyeji Ivory Coast.
Saka ambaye ni mchezaji tegemeo kwenye kikosi cha Arsenal kinachoshiriki Ligi Kuu England alionekana kufurahishwa na ushindi huo baada ya kuposti video kwenye mitandao yake ya kijamii na kuandika “Super Eagles!”.
Wazazi wote wa Saka, Adenike na Yomi, ni wazaliwa wa Nigeria, lakini akiwa ameichezea timu ya taifa ya England michezo 32 na kufunga mabao 11, kuanzia alipoitwa mara ya kwanza mwaka 2020.
Saka pia ameshapachika jumla ya mabao 50 kwenye michezo 213 aliyoitumikia Arsenal.