Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Ummy Nderiananga amesema Serikali inahitaji taasisi zake kuongeza ufanisi na tija katika utendaji wake ili kuongeza kasi ya maendeleo katika kukuza uchumi wa watanzania na Taifa kwa ujumla.

Ummy ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa Bodi ya saba ya Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) Jijini Dar es Salaam na kuitaka bodi hiyo kuwa wabunifu huku wakifanya kazi kwa uadilifu na weledi ili kuchochea ushiriki wa wananchi katika shughuli za kiuchumi nchini.

Aidha, amekumbusha kuwa mafanikio ya NEEC, yanategemea kwa kiasi kikubwa miongozo na utendaji wa Bodi kuibua na kubuni mbinu zitakazoweza kuongeza wigo wa utoaji huduma za uwezeshaji kwa weledi na kufikia wananchi wengi.

“Bodi hii inatarajiwa kutekeleza majukumu yake kwa kipindi cha miaka mitatu, hivyo ni jukumu la Bodi kuhakikisha kuwa, Baraza linafikia malengo na matarajio ya wananchi katika kipindi chote cha utendaji wake,”alisisitiza.

Waziri Ummy pia aliielekeza Menejimenti ya NEEC kuhakikisha kuwa inapokea na kutekeleza maagizo na maelekezo yote yatakayotolewa na Bodi hiyo kwa lengo la kuboresha ufanisi katika kuimarisha utoaji huduma za uwezeshaji.

Wananchi jengeni utaratibu wa kupima afya - Mchengerwa
Mashuhuda wataja sababu za ajali msafara wa Makonda