Serikali Nchini, imesema inaendelea na utekelezaji wa mradi wa kusambaza maji katika Tarafa ya Turiani toka Mwezi Desemba, 2022 kwa gharama ya Shilingi Bilioni 3.905.
Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi ameyasema hayo hii leo Februari 12 2024 Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Mvomero, Joseph Zeeland aliyetaka kufahamu ni lini Serikali itakamilisha mradi wa kusambaza Maji katika Tarafa ya Turiani.
Amesema, Shughuli zinazotekelezwa katika mradi huo ni pamoja na ujenzi wa tenki la kuhifadhia maji Kijiji cha Luamba lenye uwezo wa kuhifadhi maji lita 150,000, ujenzi wa madakio matatu ya maji katika vijiji vya Ubiri, Mlaguzi na Luamba, ujenzi wa mtambo wa kutibu maji, ujenzi wa vituo 15 vya kuchotea maji pamoja na uchimbaji wa mitaro na ulazaji wa bomba umbali wa Kilometa 70.
“Utekelezaji wa mradi huo umefikia wastani wa asilimia 45 ambapo kwa mujibu wa mkataba unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Mwezi Machi, 2024″amesema Mahundi
Amesema kukamilika kwa mradi huo kunatarajia kunufaisha wananchi wapatao 40,786 waishio kwenye Mji wa Turiani pamoja na Vijiji Tisa vya Kigugu, Mlaguzi, Mbogo, Lukenge, Mlumbilo, Luamba, Ubiri, Kwelikweji na Mafuta.