Scolastica Msewa, Gairo – Morogoro.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo – WMA, Stella Kahwa amewataka Wakulima na wazalishaji wa mbogamboga nchini, kutozidisha uzito wa kiloba au gunia la mboga kilo 100, sawa na matakwa ya sheria ya Vipimo sura na. 340 inayolenga kumlinda Mkulima na Mfanyabiashara Nchini.
Kahwa ameyasema hayo mjini Gairo, wakati akitoa elimu kwa Wakulima na Wafanyabiashara wa Mbogamboga wa Mkoa wa Morogoro na kudai kuwa ni matarajio yake kuona Wadau wa mbogamboga watazingatia sheria kwa kufungasha bidhaa zao katika uzito usiozidi kilo 100 na kwa watakaokiuka, watachukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kufikishwa Mahakamani.
Amesema Wakulima na Wafanyabiashara hao wanatakiwa kukubali kubadilika kwa kuuza au kununua mbogamboga ya kupimiwa kwenye mzani, badala ya kufungiwa katika mafungu ambayo husababisha Mkulima kupunjwa malipo kwa kuuza mboga nyingi kwa malipo kidogo au kuzidishiwa mboga wakati mizani ipo.
“Wakulima hutumia gharama nyingi katika kilimo na utunzaji wa mbogamboga shambani lakini ndio hao hao wanaishia kudhulumiwa na wachuuzi wanaowataka wawauzie mboga mboga kwenye kiloba au gunia lililojaa lumbesa ya kilo 130 jambo ambalo sio sahii kwa mujibu wa sheria,” alisema Stella.
Awali akifungua mkutano huo Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Jabiri Makame aliwataka Wakulima na Wafanyabiashara hao kuzingatia taratibu na sheria za nchi, ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza kwani Wakala wa Vipimo nchini wanatekeleza sheria za nchi, huku Mkurugenzi wa Halmashauri ya Gairo Sharifa Nabalanganya akiwataka wakubaliane na utekelezaji wa sheria ya wakala wa vipimo.
Amewasisitiza Wakulima na Wafanyabiashara hao kwenda kujifunza mbinu bora zinazowafanikisha wafanyabiashara na wakulima wa maeneo mengine kufungasha katika uzito unaotakiwa na kupata faida na kuwaahidi kuwaboreshea eneo kwaajili ya kuuza mazao yao ya mbogamboga, ikiwa ni pamoja kuwajengea choo.