Wizara ya Madini imeanza mazungumzo na Kampuni ya TAQWA-DALBIT kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa upatikanaji wa nishati ya umeme migodini na maeneo yenye wachimbaji wadogo ili kuchochea shughuli za uchimbaji madini nchini Tanzania.

Mazungumzo hayo yamefanyika Jijini Dodoma na kuongozwa na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde na Naibu Waziri Madini, Dkt. Steven Kiruswa pamoja na Menejimenti ya Uongozi wa Kampuni ya TAQA-DALBIT chini ya Meneja Mkuu, Amr Aboushad na Mkurugenzi wa maendeleo ya Biashara, Raphael Banzi.

Akiwasilisha maelezo ya awali, Amr Aboushad amesema Kampuni yao ipo tayari kuja na mpango wa uzalishaji wa umeme kupitia gesi kwa kufunga mtambo katika migodi na maeneo ya wachimbaji ambayo itasaidia kupunguza gharama za uzalishaji kwa zaidi ya nusu ya gharama inayotumika sasa.

Hatua hiyo itatekelezwa, kupitia matumizi ya mafuta ya dizeli na petroli na awamu ya pili itahusisha uzalishaji wa umeme kupitia mfumo wa umeme jua ambapo Kampuni itafunga mtambo mkubwa kwa gharama yao na kuwaunganisha wachimbaji wadogo kwa malipo ya mwezi ya matumizi ya nishati hiyo.

Akizungumza katika mkutano huo,Waziri wa Madini, Anthony Mavunde ameishukuru Kampuni ya TAQA-DALBIT kwa utayari wa kutatua changamoto ya upatikanaji wa nishati ya umeme migodini na kuagiza uongozi wa Wizara kuitisha mkutano wa haraka na wadau wote wakiwemo wachimbaji wadogo na wakubwa ili kupata fursa ya kujadiliana namna bora ya utekelezaji wa mpango huu.

Utekelezaji wa mpango huu utasaidia sana kuchochea shughuli za uchimbaji nchini Tanzania na hivyo kuongeza uzalishaji wa madini.

Dkt. Mfaume ataja malengo Mkutano Waganga Wakuu
Wauzaji Mbogamboga watakiwa kutumia mzani