Timu ya watu maalumu kutoka Klabu ya Simba SC tayari imetua nchini vory Coast kuhakikisha inatengeneza mazingira mazuri kabla ya kuwasili kwa kikosi chao katikati ya juma hili.
Simba SC itakuwa ugenini kucheza na Asec Mimosas katika mchezo wa Mzunguuko watano wa hatua ya makundi wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika ‘CAFCL’, utakaopigwa Jumamosi (Februari 23), katika Uwanja wa Felix Houphoet- Boignymjini Abidjan nchini humo.
Simba SC itaingia katika mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Wydad AC uliofanyika Desemba 19, mwaka jana Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es salaam.
Mechi ya kwanza Simba SC kukutana na Asec Mimosas timu hizo zilitoka sare ya 1-1 nyumbani.
Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba SC, Ahmed Ally amesema tayari walishatuma timu ya watu maalumu ambayo ilishatua nchini humo tangu mwishoni mwa juma lililopita.
Amesema waliamua kupeleka timu hiyo nchini Ivory Coast kuhakikisha inafanya maandalizi yakutosha kabla ya kikosi kuwasili ikiwemo kukabiliana na hujuma mbalimbali zinazoweza kujitokeza.
Ahmed amesema tayari timu hiyo ilishafika nchini humo na inaendelea na maandalizi kuhakikisha wanaandaa mazingira mazuri ya wachezaji na uongozi mzima.
Tayari tulishatuma timu ya watu maalumu ambao walishafika nchini Ivory Coast kuhakikisha wanaandaa mazingira mazuri ikiwemo kukabiliana na hujuma mbalimbali zinazoweza kujitokeza,” amesema Ahmed.
Amesema pia wachezaji wote walishaanza maandalizi ya mchezo huo mara baada ya Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB), iliposogeza mbele mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mtibwa Sugar ambao ulikuwa uchezwe jana Jumapili (Februari 18), katika Uwanja wa Jamhuri, mjini Morogoro.
Amesema wachezaji walishaanza maandalizi na wana ari kubwa kuelekea katika mchezo dhidi ya Asec Mimosas ugenini.
Amesema wachezaji, Benchi la Ufundi na baadhi ya viongozi wanatarajia kuondoka keshokutwa Jumatano (Februari 21) kwenda lvory Coast tayari kwa mchezo huo.
Amesema mchezo huo ni muhimu kwao kwani matokeo watakayoyapata yatatoa taswira nzima ya kuelekea katika hatua ya Robo Fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika ‘CAFCL’ msimu huu 2023/24.
“Maandalizi tayari yalishaanza tangu TPLB ilipotangaza kuahirisha mechi yetu dhidi ya Mtibwa Sugar na wachezaji wana ari kubwa.
“Mchezo dhidi ya Asec ni muhimu zaidi kwetu kwani ndio itatoa taswira ya kuelekea hatua ya Robo Fainali ya michuano ya msimu huu, tumejipanga vyema kuhakikisha tunapata matokeo chanya,” amesema Ahmed.
Simba SC ilianza hatua ya makundi ya michuano hiyo kwa sare ya 1-1 dhidi ya Asec, ikasuluhu mbele ya Jwaneng Galaxy, ilifungwa 1-0 dhidi ya Wydad AC na kushinda 2-0 ilipopambana na Wydad.
Katika msimamno wa Kundi B, Simba SC ipo nafasi ya pili kwa pointi tano nyuma ya Asec yenye Pointi 10 kileleni, Jwaneng Galaxy ina pointi nne wakati Wydad ikiburuza mkia na alama tatu ambapo timu zote zimeshacheza mechi nne kila moja.