Young Africans leo Ijumaa (Machi Mosi) itashuka kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Cairo, mishale ya saa 1:00 usiku (Kwa saa za Afrika Mashariki)) kuwavaa mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Al Ahly katika mchezo unaosubirivwa kwa hamu na mashabiki wengi wa soka nchini Tanzania na Misri.
Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans Miguel Gamondi, amewataka wachezaji wake kucheza bila presha na kuonyesha soka safi, katika mchezo huo.
Kocha Gamondi amesema hakuna wanachotafuta zaidi ya vita ya kuongoza Msimamo wa Kundi D, lakini tayari wameshafuzu kucheza Robo Fainali ya michuano hiyo mikubwa zaidi kwa ngazi vilabu Afrika.
Al Ahly ilifanikiwa kutinga hatua hiyo kwa kuifunga Medeama va Ghana bao 1-0 ikiwa ugenini, huku Young Africans ikiitandika CR Belouizdad ya Algeria mabao 4-0 Jumamosi (Februari 24), kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam.
Matokeo hayo yamefanya Msimamo wa Kundi A kuongozwa na Al Ahly yenye pointi tisa ikifuatiwa na Young Africans yenye pointi nane, ambazo zote zimefuzu kucheza Robo Fainali ya michuano hiyo zikiziacha CR Belouizdad na Medeama.
Kuelekea mchezo huo wa leo, Kocha Gamondi amesema wamejiandaa kucheza soka safi huku wakiwa na lengo la kusaka ushindi, lakini hataki wachezaji wake kucheza kwa presha mchezo huo.
“Ni mechi ngumu, Al Ahly ni timu kubwa na nzuri, ndiyo mabingwa wa Afrika, watakuwa nyumbani kwao mbele ya mashabiki wao, nimewaambia wachezaji wangu tayari tumeshaingia Robo Fainali, hivyo wasicheze kwa presha na wakifuata nilichowaambia tunaweza kupata kitu hapa Cairo na kuwashangaza wenyeji wetu,” amesema Gamondi.
Amesema itakuwa furaha kwao kama watamaliza mechi zao na kuongoza Msimamo wa Kundi D ,wakishika nafasi ya kwanza.
“Vita ya sasa ni nani atamaliza nafasi ya kwanza na nani atamaliza nafasi ya pili, si vita ya kufuzu Robo Fainali, tumeshapata tiketi hiyo, tutacheza kwa nidhamu huku tukisimamia malengo yetu ya mchezo,” amesema Gamondi.
Amesema Al Ahly watacheza mbele ya mashabiki wao na watataka kupata ushindi ili kuwapa furaha mashabiki wao, hivyo watacheza kwa tahadhari kubwa huku wakijipanga kutumia nafasi kwenye makosa watakayoyafanya waarabu hao.
“Itakuwa mechi nzuri sana, ni mechi ya ufundi na kuonyesha kile ambacho kila mmoja anacho, wenzetu watataka kuendeleza matokeo mazuri kwenye uwanja wao wa nyumbani na sisi tunataka kumaliza kwa heshima mechi zetu,” amesema Gamondi.
Kwa upande wa beki wa kati wa timu hiyo, Ibrahim Hamad ‘Bacca’, ameweka wazi kwenye mkutano wa wachezaji ambao haukuwa na kiongozi yoyote wamekubaliana kwenda kupambana kwa sababu wanaitaka mechi hiyo.
“Tuko vizuri, tumnejiandaa vyema kwa kupambana na kumaliza katika nafasi ya nafasi ya kwanza katika Kundi D, kwa nini tunaitaka ya nafasi ya kwanza, ni kwamba ukiangalia zile timu kubwa, kongwe, ngumu, maarufu na zenye uzoefu zinashika nafasi ya kwanza kwenye makundi, hivyo inakuwva si rahisi sana kukutana nazo za Robo Fainali, tunaitaka nafasi ya kwanza ya kundi hili tucheze na timu zinazoshika nafasi ya pili kwenye kundi lao,” amesema Bacca.
Amesema mchezo wa leo ni fainali kati yao na Al Ahly ya kuwania nafasi ya kwanza ya Kundi hilo.