Bondia wa Tanzania Seleman Kidunda leo Ijumaa (Machi Mosi) atapanda ulingoni kupigana na mpinzani wake kutoka Afrika Kusini Asemahle Wellem na swali ambalo wadau wa mchezo wa Masumbwi wanalo ni je, Mtanzania huyo ataweza kulipa kisasi?.

Ikumbukwe Wellem alitoa kipigo kwa Bondia mwingine wa Tanzania, Twaha Kiduku kwa kumpiga kwa pointi mwaka jana jijini Dar es salaam.

Awali Kidunda alisema pambano hilo ni muhimu kwake kwa ajili ya kuurejesha Tanzania mkanda wa WBF lakini pia anataka kushinda hili kumlipia kisasi Kiduku.

Pambano hilo la Raundi 12 la kuwania mkanda wa WBF linafanyika kwenye ukumbi wa Ware House, Masaki, jijini Dar es Salaam ambapo Wellem anatetea mkanda huo alioupata mwaka jana baada ya kumpiga Kiduku.

Kidunda amesema kuwa yupo tayari kwa ajili ya pambano hilo na amefanya maandalizi ya kutosha kumkabili Msauzi huyo.

“Sitowaangusha Watanzania, nimejiandaa vizuri na nina uhakika nitafanya vizuri, kikubwa naomba watu wajitokeze kwa wingi kushuhudia nikitoa kipigo,” amesema Kidunda.

Kabla ya Kidunda kupanda ulingoni, pia kutakuwa na mapambano mengine ya utangulizi ambapo bondia mwingine Mtanzania, Nassib Ramadhani atapigana na Emmanuel Nadjala kutoka Malawi.

Naye Hamad Furahisha atapigana na Ally Mwerange, Lupakisyo Shoti atapigana na Jacob Maganga, Salim Jengo atapanda ulingoni kucheza na Gray Chimkwapulo kutoka Malawi.

Aidha, Mohammed Hamad atazichapa na Aidin Muzei kutoka Uganda, Omary Sultan atapigtana na Salim Athuman, Loren Japhet atapanda ulingoni kuzichapa na Hilary Katuya kutoka Zambia.

Mkurugenzi wa kampuni ya Fay Heroes wanaoandaa mapambano hayo, Abdul Salim amesema maandalizi yamekamilika na mabondia wote kutoka nje ya nchi na mikoani wameshafika Dar es salaa tayari kwa pambano la leo Ijumaa (Machi Mosi).

CCM watoa neno kifo cha Mzee Mwinyi
Aga Khan, TMJ wasitisha huduma za NHIF