Mbali ya kuwa mechi ya leo Simba SC dhidi ya Jwaneng Galaxy ni ya kulipiza kisasi kwa upande wa Wekundu hao wa Msimbazi baada ya kuondoshwa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika hatua ya kwanza dhidi ya Wabotswana hao mwaka 2021, mechi hiyo itatoa maamuzi ya nani atatinga hatua ya Robo Fainali msimu huu 2023/24 na kuungana na Asec Mimosas, ambao tayari wamekata tiketi ya kutinga hatua hiyo.

Simba SC inaumana na Jwaneng Galaxy kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia saa 1:00 usiku kusaka ushindi tu, ili kuweza kutinga hatua hiyo bila kuangalia matokeo ya mchezo kati ya Wyadad Casablanca dhidi ya Asec Mimosas ambao nao wanacheza leo Jumamosi (Machi 02).

Timu tatu, Simba SC, Wydad Casablanca na Jwaneng Galaxy zote zina nafasi ya kutinga hatua hiyo lakini zitapaswa kuangalia ma tokeo ya kila timu kwenye mechi za leo za mwisho hatua ya makundi.

Endapo Simba SC itashinda dhidi ya Jwaneng Galax, moja kwa moja itakuwa imefuzu Robo Fainali bila kuangalia matokeo ya Wydad Casablanca, lakini endapo itapoteza itatoa nafasi kwa Wamorocco hao kufuzu kama watapata ushindi dhidi ya Asec.

Ili Jwaneng Galaxy iweze kufuzu hatua hiyo itapaswa kuifunga Simba SC na kuiombea Wydad Casablanca ifungwe na Asec.

Kocha Mkuu wa Simba SC, Abdelhak Benchikha, amesema ni mchezo muhimu kwao kuwapa furaha mashabiki wao na watanzania kwa ujuma.

Amesema wamejiandaa vizuri kwenye uwanja wa mazoezi na wachezaji wake wanafahamu umuhimuu wa mechi hiyo.

“Kazi imebaki kwa wachezaji kutekeleza yale tuliyoyafanyia mazoezi, tumejiandaa vizuri kuhakikisha tunapata ushindi, hatuangalii mechi za timu nyingine, sisi tunapambana kwenye mchezo wetu kupata ushindi,” amesema Benchikha.

Amesema katika historia ya hivi karibuni Simba SC imekuwa na rekodi nzuri ya kupata ushindi katika mechi kama hizi ambazo huwa inatakiwa ipate ushindi iweze kutinga hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini wanahitaji kuwa makini kuendeleza rekodi hiyo.

“Wapinzani wetu nao wamekuja kutafuta pointi tatu, nao wana nafasi ya kusonga mbele, lazima tuwe makini licha ya kucheza nyumbani, haya yote tumeambiana kwenye uwanja wa mazoezi,” amesema Benchikha.

Rekodi zinaonyesha kabla ya msimu ambao Jwaneng waliwatibulia kutinga hatua ya makundi, msimu wa 2018/19 Simba SC ilikutana na mazingira kama ya msimu huu katika mechi ya mwisho ya makundi dhidi ya AS Vita ya DR Congo, ambapo ilikuwa ikihitaji ushindi tu kutinga Robo Fainali na ikafanya hivyo kwa kuifunga AS Vita.

Msimu uliofuata katika mazingira kama hayo Simba SC ilichapa tena AS Vita mabao 4-1 katika mechi ambayo ilikuwa inahitaji ushindi kungia makundi.

Msimu wa 2021/2022 Simba SC ilikutana tena na mazingira kama hayo kwenye kombe la Shirikisho Afrika ikapata ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Gendarmerie na kutinga Robo Fainali ikarudia tena msimu wa 2022/2023 kwa kuifunga Horoya AC ya Guinea mabao 7-0 mechi ya mwisho na kutinga hatua ya Robo Fainali.

Kocha wa Jwaneng Galaxy, Morena Ramoreboli kuelekea mchezo wa leo amesema walikuwa hapa Tanzania miaka mitatu iliyopita na wakaondoka na pointi tatu hivyo wanataka kurudia walichokifanya.

Kapu la mabao lamfurahisha Arteta
Watoto wamtelekeza Mzazi wao wa miaka 119