Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, Jumanne Sagini ametoa siku 14 kwa Watumiaji wa vyombo vya moto kuondoa namba za magari zilizoongezwa ukubwa maarufu kama 3D na vimulimuli kwa magari yote yasiyoruhusiwa, namba zote zenye vibao vyeusi na wanaotumia namba za chasis, taa zozote pamoja na stika ambazo zimeongezwa kwa matakwa ya Wamiliki au Madereva.

Sagini ameyasema hayo wakati akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es salaam, baada ya Kikao cha Baraza la Taifa la Usalama Barabarani na kudai kuwa namba hizo hazitengenezwi na Wakala aliyepata kibali kutoka Shirika la Viwango Tanzania – TBS, bali zinatengenezwa kiholela mtaani na herufi hizo kubandikwa juu ya namba halali na kufanya zisisomeke katika umbali unaotakiwa usiopungua mita 100.

Amesema, “mambo yote yanayohusiana na Usalama Barabarani hufanywa kwa mujibu wa sheria sio utashi wa mtu mmojammoja au binafsi kwa mujibu wa usalama barabarani kuhusu matumizi ya namba yamebainishwa vizuri sana na sheria kwamba namba zinazowekwa zinatakiwa ziweje? ziwe zimeandikwa na nani? anayetambulika na nani? ziwe na ubora gani? namba hizi zote hazijawekwa kwa bahati mbaya.”

Kuhusu Ving’ora, Aidha, Sagini alisema, “Ving’ora vinatoa ishara fulani ili magari mengine yaweze kupisha na hapa nisisitize kuwa magari yanayotakiwa kuwekwa Ving’ora yanajulikana kama ya Polisi, Zimamoto ya Wagonjwa na yale yaliyopo katika misafara ya Viongozi kwahiyo kufanya hivyo bila kibali maalum ni ukiukwaji wa sheria.”

Kwa upande wake Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini ambaye pia ni Katibu wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, Naibu Kamishna wa Polisi, Ramadhani Ng’anzi alisema namba zilizoongezwa ukubwa zinapigwa marufuku kwasababu za kiusalama kwani ni lazima namba za magari lazima ziwe 2D.

Watalii wa kigeni wavunja rekodi Hifadhi ya Urithi wa Dunia
Benchikha anazitaka zote 12