Lydia Mollel – Morogoro.
Kuelekea katika madhimisho ya siku ya Wanawake Machi 8, 2024 Umoja wa Polisi Wanawake (TPF-Net), Mkoa wa Morogoro wameungana na Wanawake wa Majeshi mengine kutoa msaada wa madirisha ya Aluminium, sabuni na mito vyenye thamani ya sh 2,225,000 katika Zahanati ya Polisi Morogoro, iliyopo katika kambi ya FFU ya Boma.
Akiongea na Askari hao Wanawake kwenye mapokezi ya msaada huo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro SACP. Alex Mkama amewapongeza kwa kuchagua Zahanati ya Polisi kutoa misaada hiyo kwasababu ipo katika ujenzi na maboresho ya Wodi ya Wazazi, ili ianze kutoa huduma hiyo ambayo kwa sasa bado haijaanza.
Amesema, Zahanati hiyo ili ujenzi wake ukamilike unahitaji milioni 15, msaada huu ni sehemu ndogo tu ya mahitaji ya ujenzi hivyo amewataka wadau wengine kujitokeza na kutoa msaada ili kukamilisha ujenzi huo.
Mwenyekiti wa TPF-Net Wilaya ya Morogoro, SP. Janeth Nganda kwa niaba ya Mwenyekiti wa Mkoa ACP. Asma Shemweta amesema msaada huo ni matokeo ya kuchangishana fedha kwa Wanawake wote waliopo kwenye TPF-Net Mkoa kutoka kwenye mishahara yao, ili kuwapa sapoti Wanawake wenzao wanaotarajia kupata watoto wapate huduma bora itakayo linda afya zao.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Zahanati hiyo, SP Mariam Masalu ametoa shukran zake za dhati kwa Askari wa TPF-Net na kuahidi kutumia vifaa hivyo kama ilivyokusudiwa.
Umoja huo wa Majeshi, ulianza kwa matembezi ya pamoja kutokea Kituo Kikubwa cha Polisi kupitia Mjini kati mpaka Zahanati ya Polisi huku wakiinadi kauli mbiu ya siku ya Wanawake Duniani isemayo, “WEKEZA KWA WANAWAKE KURAHISISHA MAENDELEO YA TAIFA NA USTAWI WA JAMII”.