Baada ya ukimya wa muda mrefu, Mwenyekiti wa Klabu ya Simba SC, Murtaza Mangungu, ameibuka na kutangaza mipango kabambe ya kuiwezesha klabu hiyo kufuzu Nusu Fainali kisha fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
Mangungu amejitokeza hadharani huku akisema kuwa kutoonekana kwake katika matukio mbalimbali ya klabu, kunatokana na kuwa na wawakilishi tofauti ambao kila mmoja ana uwezo wa kuizungumzia, kufanikisha kazi za klabu.
Akizungumza jijini Dar es salaam, Mangungu amesema uongozi uliopo unafanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na wadau wakubwa wa klabu na ndio maana timu inafanya vizuri.
“Usiponiona mimi mahali tambua kuwa kuna maagizo nimetoa kwa wengine na yanafanyiwa kazi, ndio maana mnaiona Simba inazidi kufanya vyema na hakuna migogoro, sio lazima nionekane kila mahali.” amesema Mangungu.
Mwenyekiti huyo amesema wapo kazini hivyo Mashabiki wapunguze kuwalalamikia viongozi na wachezaji, kwani kuna wakati wanashindwa kufanya kazi kwa kuhofia kelele.
Kuhusu mchakato wa mabadiliko ya klabu, Mangungu alisema taratibu za kufanikisha mchakato huo zinaendelea, huku klabu ikifuata taratibu na sheria za nchi.
Ameongeza kwa kuwataka Mashabiki na Wapenzi wa Simba SC kutokuwa na hofu na timu yao kwani mipango inaendelea kusukwa na kuifanya iwe bora barani Afrika.
Bayern Munich kuizidi kete Liverpool
Jumamosi (Machi 02), Simba SC ilifuzu hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika baada ya kuifunga Jwanerng Galaxy ya Botswana mabao 6-0, katika mchezo wa hatua ya makundi uliochezwa Uwanja wa Mkapa, Dar es salaam.
Simba ilianza mechi za kundi B kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Asec Mimosas kabla ya suluhu na Jwaneng Galaxy, kisha ikafungwa bao 1-0 dhidi ya Wydad Casablanca, iliichapa mabao 2-0 Wydad Casablanca na kutoka sare ya bao 1-1 na Asec Mimosas kabla ya kupata ushindi mnono wa mabao 6-0 dhidi ya Galaxy.