Watu saba wamefikishwa mbele ya Mahakimu watatu tofauti katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni, wakikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka manne, yakiwamo ya kusafirisha Sukari na Mafuta ya kupikia kwa magendo, vyote vikiwa na thamani ya Shilingi milioni 10.7.

Washtakiwa hao, pia wameshtakiwa kwa kosa la kukwepa ushuru chini ya kifungu 148(e) cha sheria ya forodha, kusafirisha mizigo ya magendo kushindwa kuwasilisha nyaraka za bidhaa za magendo na kukutwa na bidhaa za magendo

Kwa pamoja walisomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Veneranda Kaseko, Mahakimu Wakazi, Nabwike Mbaba na Ramadhani Rugemalira.

Akisoma hati ya mashtaka Wakili wa Serikali Anderson Lukosi akisaidiana na wakili kutoka TRA, Auni Chilamula amewataja washtakiwa hao kuwa ni Mfanyabiashara Mustapha Bakari (30), Mkazi wa Kunduchi, Mafundi Mohamed Nassor (25), Abdulmajid Kheri (17) na dereva Erick Solomon Mwagemba (25).

Wengine ni dereva Justin Mollel (35), Wavuvi Mbaraka Mwanjovu (23) na Hamad Hamad maarufu Katoto (23).

Mbele ya Hakimu Nabwike Mbaba, washtakiwa Nassoro na Kheri wanadaiwa Februari 11, mwaka huu maeneo ya Kunduchi Wilayani Kinondoni, walikutwa wakiingiza mifuko 20 ya Sukari kwa kutumia njia ya magendo bila ya kulipa kodi na kukwepa ushuru wa Sh. 2,335,697.93 kinyume na sheria.

Inadaiwa siku hiyo pia washtakiwa hao walikwepa ushuru kwa kuingiza mifuko 20 ya sukari kwa kutumia gari lenye namba za usajili T 956 BBF, huku pia wakishindwa kuwasilisha nyaraka za bidhaa za magendo pamoja na kukutwa na bidhaa za magendo.

Mbele ya Hakimu Kaseko, Erick anadaiwa kusafirisha mifuko 20 ya sukari kupitia bandari bubu na kukwepa ushuru wa Sh 2,335,697.93.

Mbele ya Hakimu Rugemalira, washitakiwa Mollel, Mwanjovu na Hamad, wanadaiwa kuwa, Februari 11 mwaka huu maeneo ya Mtongani – Kunduchi walisafirisha madumu 100 ya mafuta ya kupikia kupitia bandari bubu na kusababisha ukwepaji wa ushuru wa Sh 4,022,113.

Adaiwa kuchoma chanjo 217 za Uviko-19
Mangungu: Msihofu Simba inakwenda Nusu Fainali