Baada ya kurejea nchini kuendelea na kibarua chake, Kocha Mkuu wa Simba SC, Abdelhak Benchikha, amesema Waarabu wa Misri ‘Al Ahly’ ndiyo wanaihofia Simba SC na wamekuwa na presha kutokana na kupangwa kwa mara nyingine katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Simba SC imepangwa kucheza dhidi ya Al Ahly katika ya hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, mechi ya kwanza lkichezwa kati ya Machi 29 na 30, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam na marudiano yakifanyika Misri kati ya Aprili 5 hadi 6, mwaka huu.
Akizungumza jijini Dar es salaam, Benchikha, amesenma Al Ahly inafahamu inakutana na mpinzani mgumu kwao, hivyo anatarajia mechi zote mbili zitakuwa na ushindani.
Benchikha amesema Al Ahly hawajapenda kukutana na Simba SC kwa sababu timu hizo zinafahamiana kama zinacheza ligi moja kutokana na ratiba kuwakutanisha mara kwa mara kuanzia hatua tofauti.
“Al Ahly wanajua wanakuja kukutana na mpinzani mgumu kwa kiasi gani, na Simba SC itakwenda kupigania nafasi ya kutinga hatua ya Nusu Fainali na sio kuhofia hadhi yao.
“Tunatakiwa kujipanga kwenda kuthibitisha kwa nini tupo katika klabu 10 bora Barani Afrika kwa kushindana na klabu namba moja na bila hofu. Kila kitu kinawezekana, hatuna presha nao kwa sababu tunaijua na tutapambana.”
Kocha huyo aliyerejea nchini akitokea kwao kushiriki mafunzo ya siku tano ya kuongeza ujuzi, amewataka Wanachama na Mashabiki wa Simba SC kujiandaa kwenda kuishangilia timu hiyo kwa ajili ya kuwashangaza Waarabu hao.
“Nawaomba mashabiki wa Simba SC msiogope kuja uwanjani, njooni, tumejipanga na tumejiandaa kupambana nao na tutawashangaza,” amesema Benchikha
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba SC, Imani Kajula, amesema kujuana kwa wachezaji wa timu zote mbili kunatokana na kukutana mara kwa mara, hali hiyo ndiyo kunaifanya mechi hiyo kuwa na ahueni kwao.
“Itakuwa mechi ngumu sababu ya timu kujuana, lakini pia inatupa ahueni kwetu, wachezaji hawana presha nao, hivi karibuni tu tumecheza Cairo kwenye African Football League,” amesema Kajula.
Miezi mitano iliyopita, Simba SC na Al Ahly walikutana katika michuano mipya ya African Football League na Wekundu wa Msimbazi iliondolewa kikanuni.
Katika mechi ya kwanza iliyochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Oktoba 21, mwaka jana, timu hizo zilitoka sare mabao 2-2 na waliporudiana Oktoba 24, zikatoka tena sare ya bao 1-1, na Simba SC kutolewa kwa kanuni ya mabao ya ugenini.
Pia zilikuwa pamoja kwenye hatua za makundi msimu wa 2018/19 zikiwa Kundi D na zote zikasonga mbele hatua ya Robo Fainali, AI Ahly ikiongoza kundi, Simba SC ikifungwa mabao 5-0 ugenini na kushinda bao 1-0 nyumbani.
Mara nyingine tena ilikuwa hatua ya makundi msimu wa 2020/21, kila timu ikishinda bao 1-0 nyumbani, zote mbili zikisonga mbele, Simba SC ikiongoza kundi hilo.