Malaysia imepewa Pauni milioni 100 (sawa na zaidi ya Sh bilioni 324) ili kuiwezesha nchi hiyo kuandaa Michezo ya Jumuiya ya Madola ya mwaka 2026.
Michezo hiyo kwa sasa haina mwenyeji baada ya jimbo la Australia la Victoria kujitoa kuiandaa Julai mwaka jana kwa sababu ya ongezeko la gharama za michezo hiyo.
Baraza la Olimpiki la Malaysia linasema lilipokea mwaliko rasmi kutoka Shirikisho la Michezo ya Jumuiya ya Madola (CGE) kuchukua nafasi ya Victoria kama mwenyeji mwezi uliopita.
CGF inasema iko katika “majadiliano ya kina” na waandaaji hao watarajiwa.
Taarifa kwenye tovuti ya Baraza la Olimpiki la Malaysia (0CM) ilisema kiasi hicho cha fedha kitasaidia maandalizi na michezo hiyo ya mwaka 2026.
Malaysia iliwahi kuandaa michezo hiyo hapo awali, katika mji mkuu wa nchi hiyo Kuala Lumpur mwaka 1998.
Rais wa Chama cha Michezo ya Jumuiya ya Madola ya Malaysia, Mohamad Norza Zakaria alisema fursa ya kuwa mwenyeji mwaka 2026 ilikuwa fursa ya mara moja ambayo itasaidia kuendeleza mafarikio ya mwaka 1998 na kuirejesha tena nchi katika ramani ya michezo duniani.
Msemaji wa CGF aliiambia BBC Sport kwamba Pauni hizo milioni 100 za msaada wa kifedha na wa kimkakati zimetolewa kwa waandaaji watarajiwa kama sehemu ya kuisaidia Malaysia baada ya kujiondoa kwa Victoria.
Taarifa ilisomeka: “CGF iko katika majadiliano ya kina ya siri na waandaaji watarajiwa, ili kupata suluhu ya Michezo ya 2026 ambayo inawatia moyo wanariadha na kusaidia kubadilisha michezo kuwa mtindo endelevu.
“Malaysia ina rekodi nzuri ya kuwasilisha matukio ya michezo na Michezo ya Jumuiya ya Madola ya 1998 huko Kuala Lumpur ilifanikiwa kwa kiasi kikubwa.
“Tunakaribisha mapendekezo ya kibunifu na tuko katika majadiliano chanya na waandaaji watarajiwa.”
Michezo ya Jumuiya ya Madola ni tukio linaloshirikisha michezo mingi na iliwahi kufutwa mara mbili tu, mwaka 1942 na 1946, kwa sababu ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia.