Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imemtaka Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa kuhakikisha anaisimamia Wakala wa Majengo – TBA, kuendeleza maeneo yao na kupata hatimiliki ya maeneo hayo ili kuepusha migogoro ya ardhi kati ya Wakala huo na Halmashauri za Wilaya na Miji.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Selemani Kakoso ameyasema hayo wakati wa ziara ya ukaguzi wa Kamati hiyo kwenye mradi wa jengo la makazi kwa watumishi wa umma, eneo la Ghana Kota jijiji Mwanza na kuridhishwa na utekelezaji wa mradi huo, ambao kwa sasa umefika asilimia 50.

Aidha, Kakoso amempongeza Waziri Bashungwa kwa kusimamia kikamilifu zoezi la ukusanyaji wa madeni kwa Taasisi za Serikali zinazodaiwa na TBA na hivyo kusisitiza kuongeza kasi ya ukusanyaji wa madeni ili kuwezesha Wakala huo kupata fedha na kutekeleza miradi mingi zaidi nchini.

Kakoso ameisisitiza TBA kuwa wabunifu kwa kujenga majengo ambayo yatakuwa na mvuto wa kibiashara na pia kujenga katika maeneo ambayo yana uhakika wa kupata wapangaji pamoja na kuanzisha utaratibu wa kujenga majengo ambayo watakuwa wanayauza.

Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema kuwa Serikali kupitia TBA imejipanga kuendelea kusaidia watanzania kwa kuwajengea makazi bora na ya kisasa.

“Katika eneo hili la mradi kulikuwa na familia nne ambazo zilikuwa zikiishi, lakini kwa utaratibu huu badala ya familia nne za awali sasa familia 14 zinaweza kuishi katika eneo hili ambalo jengo lake ni bora, la kisasa na lenye viwango vya kimataifa”, amesisitiza Bashungwa.

Amesema kuwa mradi huo ni kielelezo cha kuonesha namna ambavyo Wizara yake kupitia TBA ilivyojipanga kuhakikisha kuwa maeneo yote ambayo wamepewa na Serikali wanayaboresha na kuleta huduma bora kwa jamii.

Awali akitoa taarifa ya mradi huo, Mtendaji Mkuu wa TBA, Arch. Daudi Kondoro amesema mradi wa Ghana Kota ni moja ya utekelezaji wa maelekezo ya Serikali juu ya uendelezaji wa maeneo ya Kota nchini ambapo mradi huo unatekelezwa kupitia mapato ya ndani ya Wakala huo ambapo ujenzi unagharimu Shilingi Bilioni 6 na unatarajiwa kukamilka mwezi Julai, 2024.

Malaysia yalamba Bilioni 324 Jumuia ya Madola
Dkt. Kikwete ashinda Tuzo Viongozi bora amani