Wawekezaji wa Viwanda Nchini, wameshauriwa kutumia Gesi asilia ili kupunguza gharama za bei ya Nishati hali ambayo itawasaidia kuzalisha zaidi na kutoa huduma bora ya bidhaa zao.
Ushauri huo, umetolewa hii leo Machi 16, 2024 jijini Dar es Salaam na Kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, chini ya Mwenyekiti wake David Mathayo wakati ilipotembelea Viwanda vinavyotumia Gesi cha MMI Steal kinachozalisha mabati na Tanpack kinachozalisha tishu.
Amesema, “Watanzania wanaotumia gesi ni wachache kwahiyo TPDC waendelee kusambaza gesi hiyo kwa wingi ili na watu waendelee kuitumia kusaidia utunzaji wa mazingira, joto linazidi ni kwasababu ya kutumia nishati isiyo safi inayoharibu si mazingira bali na hali ya hewa.”
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, James Mataragio amesema Serikali imejipanga kuhakikisha gesi inawafikia Wananchi ambapo wanatarajia kufanya uunganishaji wa gesi Majumbani na kwenye Viwanda vyote ili kukidhi mahitaji.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Petroli Nchini – TPDC, Mussa Makame amesema utaratibu wa usambazaji wa gesi kwa mujibu wa sheria ya gesi ya mwaka 2015 inawashirikisha watu binafsi kwenye uwekezaji na kwamba ni matarajio yao kuona malengo yanafikiwa.