Ni kumbukizi ya miaka mitatu tangu kifo cha Rais wa awamu ya tano, Hayati John Pombe Joseph Magufuli, kilichotokea Machi 17, 2021 jijiji Dar es Salaam.
Katika kumbukizi hii, Mkuu wa Majeshi Mstaafu, Jenerali Venance Mabeyo amefanya mahojiano na Waandishi wa Habari wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali – TSN, ambapo amesema siku moja kabla ya kifo Magufuli, alimwita na kumwambia anajua hawezi kupona na hivyo awaagize Madaktari wamrudishe nyumbani.
Amesema, “aliniita CDF njoo siwezi kupona, waamuru hawa Madaktari wanirudishe nyumbani. Nikamjibu Mheshimiwa sina Mamlaka hayo, suala la Afya sio la CDF, naomba ubaki Madaktari watatuambia.”
Mabeyo ameongeza kuwa, Machi 17, 2021 majira ya saa 8 mchana, Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama waliambiwa hali ya Rais Magufuli imebadilika na ilipofika saa 12:30 Jioni aliaga dunia.
“Wakati anafariki, Makamu wa Rais (wakati huo na Rais wa sasa) Dkt. Samia Suluhu Hassan alikuwa Mkoani Tanga, Katibu Mkuu Kiongozi alikuwa Dodoma na Waziri Mkuu alikuwa Mkoani pia. Tuliwapigia Waziri Mkuu na Katibu Mkuu kiongozi kuwaomba waje haraka Dar es Salaam bila kuweka wazi sababu ya kuwaita,” alisema Mabeyo.
Amesema, “walipofika niliwaweka wazi kuwa Mhe. Rais (Hayati Magufuli) ameshafariki, tukaanza kushauriana tunafanyaje, nani anapaswa kutangaza habari hizi katika vyombo vya habari ili wananchi wajue.”
“Na pia tukaanza kutafuta katiba kuona inasema nini, mtu pekee anapaswa kutangaza kwenye vyombo vya habari ni Makamu Rais na wakati huo alikuwa Tanga, yalifanyika mawasiliano mengine akiwa Tanga ili ajulishwe,” alisimulia Mabeyo.
“Lakini pia familia yake ilikuwa haijui na iko hapa Ikulu Dar es Salaam na haijaambiwa na mama yake yuko Chato na hatuwezi kumwambia kwa simu, nani anakwenda kumwambia mama Magufuli, ili kabla ya kutangazwa wao wajue na wasipate taarifa kupitia vyombo vya habari,”
“Tuliwapata watu kwenda Ikulu na mwingine kwenda Chato kwa kutumia charter plane (ndege maalum). Ndio maana uliuona alifariki saa 12:30 jioni na tukachelewa kutangaza, hadi kuja kutangaza saa 5 usiku,” ameeleza Jenerali Mstaafu Venance Mabeyo.
Aidha, amesema, “kulikuwa na mawazo mawili baada ya kifo cha Hayati Rais Magufuli, je Rais mteule (kwa mujibu wa katiba ambaye nk Makamu wa Rais wa wakati huo) aapishwe kabla ya kuzika au baada ya kuzika? kulikuwa na mjadala hapo, ikaja logic (mantinki) kwamba kuna Marais watatoka nje kuja kuzika, je watapokelewa na Rais au na Makamu wa Rais?”
“Tukaona ni lazima Rais, hivyo tukafikia maamuzi Makamu wa Rais aapishwe kuwa Rais,” aliongeza Mkuu huyo wa Majeshi Mstaafu, Jenerali Venance Mabeyo.