Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mohamed Mchengerwa amewataka Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa nchini kusimamia na kutatua migogoro ya ardhi katika maeneo yao.

Mchengerwa ameyasema hayo katika ukumbi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Njedengwa Jijini Dodoma, wakati akihitimisha kikao kazi cha kujadili Sura ya Mipango na Bajeti ya Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Tume ya Utumishi wa Walimu, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa fedha 2024/25.

Amesema, suala la migogoro ya ardhi limekuwa kero kubwa kwa wananchi na njia pekee ni Viongozi hao wa mikoa kuisimamia na kutatua wakishirikiana na wataalam wao.

“kuendelea kuwepo kwa migogoro ya ardhi katika maeneo yenu inadidimiza shughuli za maendeleo kutokana na muda na rasilimali nyingi kutumika kushughulikia migogoro hiyo, tumieni busara na wataalamu mlionao katika Ofisi zenu katika kusuluhisha migogoro iliyopo kwa kuzingatia Sheria za Nchi, Kanuni na Taratibu” alisema Mchengerwa.

Aidha, amewataka Wakuu wa Mikoa kuwafuatilia baadhi ya viongozi wa Mkoa na Wilaya ambao hawafuati sheria katika kuzuia utekelezaji wa tuzo za mabaraza ya ardhi na nyumba ya Kata na Wilaya katika kutolewa kwa tuzo ya ushindi, suala ambalo limekuwa likilalamikiwa na wananchi na mahakama yenyewe ambapo amewashauri kuwatumia vyema wanasheria wao ili kuepusha malalamiko na migongano na mhimili wa mahakama.

 

Katika hatua nyingine Mchengerwa amemwagiza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI,  Adolf Ndunguru kuwasiliana na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora ili kuhakikisha Wakuu wa Mikoa wanapewa mamlaka ya kushughulikia kero za ardhi kwenye mikoa yao kwani pia ni msingi wa Madaraka Mikoani (Decentralization by Devolution) badala ya Maafisa Ardhi kuwa chini ya Wizara ya Ardhi jambo linalosababisha viongozi hao kushindwa kutatua migogoro mingi ya ardhi.

21 wapoteza maisha kwa ajali ya Basi kugonga Lori la mafuta
Mabeyo: Magufuli aliniita, alijua hatapona