Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Iringa – IRUWASA, imeandika historia mpya kwa kupata tuzo baada ya kuwa ya kwanza katika kundi la pili lenye wateja wengi, (kuanzia 20,000 – 200.000), kwa mara ya pili.
Tuzo hizo zimetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mwajuma Waziri wakati wa uzinduzi wa Taarifa ya Utendaji wa Mamlaka za Maji Safi na Usafi wa Mazingira, kwa kipindi cha Mwaka 2022/23 ambapo tuzo hizo zilikuwa zikitolewa kwa Mamlaka zote za maji Nchini.
Akiongea mara baada ya ushindi huo Mkurugenzi Mkuu wa IRUWASA, Mkoa wa Iringa, David Palanjo amesema siri ya kushinda kwao ni ushirikiano mzuri kutoka ngazi ya juu hadi chini.
Amesema, “ushirikiano mzuri unaanzia juu na juu kukiwa na Ushirikiano mzuri basi pia chini kutakuwa na Ushirikiano mzuri hivyo basi,Lakini pia busara kutoka kwa watendaji, kuangalia nini wizara ya maji inatuelekeza.”
Kuhusu suala la upatikanaji wa Maji muda wote katika Mkoa wa Iringa, Palanjo amesema kwao limekuwa ni jambo la kawaida kwani upatikanaji wa Maji upo kwa masaa 24 kwa siku saba za wiki.
“Na hata ikitokea usiku kuna changamoto ya hitilafu mahali lina tatu kuwa muda huo huo, na watu wanapata huduma kwa muda huo, na hata hitilafu ikitokea na tukashindwa kutatua basi hilo suala linakuwa la umeme hivyo TANESCO watahusishwa,“ aliesema Palanjo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Maji Iringa, Monica Mbega amesema ushirikiano mzuri ndio chanzo cha wao kushinda tuzo hiyo ya maji ikiwemo suala la kuheshimiana wenyewe kwa wenyewe, kusikilizana na kufata maelekezo kwa wakati.
“Lakini pia utendaji wetu wa kazi, bodi ukitoa maagizo na menejimenti ikifuatilia kwa uzuri kwa kushirikiana vizuri basi lazima kuwe na utendaji mzuri wa kazi, tunatii, kueshimiana na kushirikiana baina yetu,” alisema Mbega.