Kiwanda cha Kibaiolojia kinachomilikiwa na Serikali cha Tanzania Biotech Product limited – TBPL, kilichoko Kibaha mkoani Pwani kimeingia rasmi mkataba wa miaka mitatu na kampuni ya JJ Agricultural Ltd ya kusambaza Dawa mpya za viuatilifu hai, ambavyo vitatumika katika kupambana na wadudu dhurifu wa mazao mbalimbali ya Kilimo, ikiwemo Pamba, Mahindi, Matunda na Mbogamboga.

Taarifa ya Kitengo cha Mawasiliano na Masoko, Shirika la Taifa la Maendelo – NDC, imeeleza kuwa katika mkataba huo ambao umesainiwa hii leo Machi 19, 2023 Kiwandani hapo Kibaha mkoani Pwani, upande wa kampuni ya TBPL umewakilishwa na Meneja Mkuu wa kiwanda hicho, Rafael Rodriquez na kwa upande wa JJ Agricultural Ltd, imewakilishwa na Mkurugenzi wa kampuni hiyo Mhandisi, James Kilaba.

Akizungumza mara baada ya kukamilika kwa zoezi la kutiliana saini mkataba huo, Meneja Mkuu wa kiwanda hicho, Rafael Rodriquez ameonyeshwa kufurahishwa na makubaliano waliyofikia na kampuni ya JJ Agricultural Limited ambapo amebainisha kuwa hatua hiyo ni mafanikio makubwa katika kuhakikisha kuwa wananchi wanapata fursa ya kufikiwa na bidhaa hiyo katika maeneo mbalimbali nchini.

Amesema, “tunatambua changamoto inayowakabili wakulima ya uwepo wa wadudu dhurifu katika mazao yao makabaliano haya yanakwenda kuwasaidia wakulima katika kupatikana kwa dawa hii hali itakayowafanya wakulima kuongeza tija na uzalishaji katika mazao yao.”

Rodriquez pia ametumia fursa hiyo kubainisha sifa za dawa hizo kuwa zimetengenezwa kwa namna ya viuatilifu hai, ikilinganishwa na dawa zingine zisizo za kibaolojia kwa kuwa zinapelekea madhara watumiaji kama vile magonjwa ya kansa pamoja na kuharibu mazingira, huku akiwataka Mawakala zaidi kuendelea kujitokeza kwa wingi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa kampuni ya JJ Agricultural Ltd, Mhandisi James Kilaba ameishukuru TBPL kwa kufikia makubaliano ya kusaini mkataba huo huku akiomba kupewa ushirikiano katika kipindi chote cha utekelezaji wake ambapo miongoni mwa kazi zitakazofanywa na kampuni hiyo ni pamoja na kuhakikisha wanaandaa mashamba darasa katika maeneo mbalimbali.

Mkataba huo wa miaka mitatu na kwa kuanzia dawa hizo zinatarajia kupatikana katika mikoa ya Dar es salaam Pwani, Morogoro, Mwanza, Geita, Simiyu, Shinyanga, Iringa, Dodoma Singida, Katavi pamoja na Tanga na utahusisha pia utoaji wa mafunzo ya namna bora ya kutumia dawa hizi ambao utakuwa unafanywa na wataalam kutoka katika kiwanda cha TBPL.

Kiwanda cha Kibaolojia cha TBPL ni cha pekee kilichopo nchini na barani Afrika, ambacho kinamilikiwa na Serikali kikizalisha dawa za kibaolojia hapa nchini ambapo kinazalisha dawa za Viuadudu vya kupambana na Maleria (biolarvicides), ambapo kwa sasa mara baada ya kubaini uwepo wa changamoto za wadudu dhurifu katika kilimo imeanza rasmi uzalishaji wa dawa za viuatilifu hai vya kilimo (biopesticides) ambavyo ni bora na rafiki wa mazingira.

Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Machi 20, 2024
IRUWASA yaandika historia mpya, yabeba tuzo mshindi wa kwanza