Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amemuelekeza Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini katika Wizara yake, kufuta jumla ya maombi na leseni za Madini 2,648 kwa wamiliki ambao hawajayaendeleza maeneo yao, sehemu mbalimbali nchini, ili kupisha waombaji wengine kupata fusra ya kuyamiliki na kuyafanyia uendelezaji.
Mavunde ameyasema hayo hii leo Machi 22, 2024 wakati akiongea na Vyombo vya Habari na kuongeza kuwa wapo watu sita wanaoshikilia maeneo yenye ukubwa wa hekari Milion 13, sawa na mikoa minne ya Kilimanjaro na hawayaendelezi, huku akitoa onyo kali kwa wamiliki wa akaunti za uombaji na usimamizi wa Leseni kwa njia ya mtandao, wenye matumizi mabaya ya kimfumo juu ya umiliki wa maeneo.
Amesema, “kumekuwa na baadhi ya Wamiliki wa Leseni ambao wamekuwa hawazingatii utekelezaji wa majukumu yao ya umiliki wa Leseni kwa mujibu wa sheria ya Madini sura ya 123, miongoni mwa makosa ya mara kwa mara ni pamoja na Wamiliki wa leseni kutoyaendeleza, kutolipa ada na badala yake kuyamiliki.”
“Tume ya Madini imetoa haki za makosa kwa jumla ya Leseni 59 hai za utafutaji wa Madini kwasababu wamiliki wake hawajatekeleza masharti ya umuliki wa leseni husika, imebainika kuwa hadi Februari 2024 kuna jumla ya maombi 2,180 ambayo hayajalipiwa ada stahiki za maombi na kuna uwepo wa maombi 409 ya muda mrefu, ambayo wamiliki wake wamelipa ada lakini hawajawasilisha nraraka muhimu,” amesema Mavunde.