Benchi la Ufundi la Mabingwa wa Soka Tanzania bara Young Africans, limesema wachezaji wake wana morali nzuri kuelekea mchezo wa Mkondo wa kwanza wa Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika (CAFCL).
Young Africans ilipoteza mchezo wa Ligi Kuu mwishoni mwa juma lililopita kwa kufungwa 2-1, dhidi ya Azam FC lakini imesisitiza kujipanga ili kuhakikisha inashinda mchezo wake wa kimataifa mwishoni mwa juma lijalo.
Katika michuano ya Kimataifa Young Africans itakuwa mwenyeji wa mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Robo Fainali, Ligi ya Mabingwa Baranbi Afrika kwa kuikaribisha Memelodi Sundowns, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam Jumamosi (machi 30) saa 3.00 usiku.
Kocha wa Young Africans, Miguel Angel Gamondi amesema alidhani atakuwa na mtihani mgumu kuwajenga kisaikolojia wachezaji wake baada ya kichapo dhidi ya Azam FC, lakini amekutana na kitu tofauti kutokana na kikosi chake kuwa morali nzuri na kipo tayari kwa kupambana dhidi ya Mamelodi Sundowns.
“Mpira ni mchezo wa makosa, nyota wangu walikosea kidogo na wakaadhibiwa, wameahidi kupambana kwa kurudisha furaha kwa mashabiki wetu, kitu ambacho nimekifurahia na naamini kitaongeza chachu ya ushindani katika mechi yetu ya Ligi ya Mabingwa Afrika,”
Gamondi amesema baada ya kuona wachezaji wake wamekubali kupoteza na kukubali kuendeleza mapamnbano tayari kwa mchezo unaofuata, amekaa nao na kuwapa namna ambavyo wanatakiwa kufanya kuweza kuanza vizuri mchezo wao wa Jumamosi (Machi 30).
“Huwa napenda kila mchezaji katika kikosi changu kuwa tayari, kwani muda wowote anaweza kutumika kulingana na mahitaji ya mchezo, kila mchezaji kwangu ana nafasi na ndio maana huwa tunawaandaa mazoezini, anayeonakana kufanya vizuri katika mpango wangu hupewa nafasi,” amesema.
Amesema inapotokea mpango wa kwanza umeshindikana, ndipo anaangalia nini kinapaswa kufanyika, kama waliopo wanatosha au aongeze nguvu kwa mchezaji aliyepo benchi.
Katika hatua nyingine Gamondi amewataka wachezaji wake kuongeza uwajibikaji uwanjani na kujiongeza kimbinu kulingana na mpinzani anapobadili mbinu zake kukwepa mitego.
Amesema hawapaswi kubweteka wanatakiwa kufanya vizuri zaidi kutokana na uwepo wao katika mashindano ya kimataifa na wana amesema.