Majaji wa Mahakama ya Brazil wameunga mkono hukumu ya Mahakama ya Italia ya ubakaji inayomuhusu mshambuliaji wa zamani wa AC Milan na Timu ya Taifa ya Brazil, Robinho, na kuongeza lazima atumike kifungo cha miaka tisa jela.
Majaji wa mahakama ya juu zaidi ya Brazil walipiga kura 9 kwa 2 kuthibitisha hukumu ya mshambuliaji huyo wa zamani wa Real Madrid kwa na Manchester City.
Robinho mwenye umri wa miaka 40 alihukumiwa Italia kifungo cha miaka tisa jela kwa kushiriki katika kundi la unyanyasaji wa kingono mwaka 2013 alipokuwa akiichezea AC Milan.
Brazil haiwakabidhi raia wake kwa nchi nyingine kutumikia kifungo, hivyo ikaifanya Italia kutafuta kifungo katika taifa lake.
Uamuzi huo uliamuliwa na mahakama ya juu zaidi ya Brazil yenye jopo la majaji 15 katika mji mkuu Brasilia na kumtaka Robinho kutumikia kifungo hicho.
Wakili wa Robinho, José Eduardo Rangel de Alckim, alisema atakata rufaa dhidi ya uamuzi huo katika mahakama ya juu ya Brazil na ataomba mchezaji huyo akae nje ya gereza wakati wa mchakato wa kukata rufaa.
“Robinho yupo na yuko tayari kufika wakati wowote mbele ya majaji na akifika hapo atatii. Hatapinga,” alisema Alckim.
“Wasiwasi wetu wa kwanza ni kusitisha agizo la kukamatwa mara moja. Tutaomba hukumu hiyo itekelezwe baada ya uamuzi wa rufaa kufanywa.”
Jaji wa kwanza kuupiga kura, Francisco Falcão, alisema Robinho anafaa kutumikia kifungo chake Brazil.
Aliongeza mchezaji huyo wa zamani hawezi kuachwa bila kuadhibiwa na msuguano wa kidiplomasia kati ya Brazil na Italia unaweza kutokea iwapo adhabu hiyo haitatolewa.
“Hakuna kikwazo kuthibitisha utekelezaji wa hukumu yake. Ilithibitishwa na mahakama ya Milan ambayo ndiyo mamlaka yenye uwezo katika kesi hii,” aliongeza Falcão
“Hukumu ni ya mwisho. Mshtakiwa hakushtakiwa bila kuwapo Italia alikuwa na uwakilishi.”
Robinho anaishi Santos, nje ya Sao Paulo na hati yake ya kusafiri inashikiliwa na Mamlaka ya Brazi tangu Machi, mwaka jana.
Ameendelea kukana kosa na kusisitiza mahusiano yake ya kimapenzi na mwanamke huyo katika baa ya Milan yalikuwa ya maelewano.