Angela Msimbira – Serengeti.
Kamati ya Kudumu ya Bunge za Serikali za Mitaa (LAAC) imeiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kuhakikisha inafuata sheria,kanuni na taratibu za ununuzi kila inapoanza kutekeleza miradi ya ujenzi katika Halmashauri hiyo.
Agizo hilo limetolewa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa, Staslaus Mabula alipokagua mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Serengeti, Mkoani Mara
Mabula amesema kazi ya ujenzi wa hospitali hiyo kimefanyika kiufundi na ustadi wa hali ya juu lakini utaratibu wa ununuzi haukufuatwa.
Amesema kuwa kwenye ujenzi wa hospitali hiyo taratibu nyingi za ununuzi zimekiukwa ikiwemo ununuzi wa vifaa vya ujenzi kukunuliwa kwa wazabuni, wasio idhinishwa na wakala la ununuzi serikali GPSA, nukuu za bei kutoidhinishwa na Bodi ya Zabuni ya Halmashauri
Kamati imeiagiza Halmashauri kuhakikisha inajibu hoja 10 za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2021/22 na kuhakikisha wanawasilisha vielelezo muhimu vinazohitajika ili kufunga hoja hizo.
Aidha Kamati imemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kuhakikisha anasimamia ukusanyaji wa Mapato na kuhakikisha fedha hizo zinapelekwa benki kwa kuwa bila kufanya hivyo ni kukiuka utaratibu wa fedha za Serikali hivyo haitosita kuielekeza Serikali kuwachukuli hatua watumishi wanaokiuka utaratibu wa ukusanyaji wa mapato