Uamuzi wa kuwepo kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar, ulizingatia kutanguliza mbele usalama wa maisha ya watu, maslahi, utulivu na mstakabali mwema wa Zanzibar, Wazanzibar na Watanzania wote kwa ujumla, kuliko vyama vya siasa.
Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi alipokuwa akizungumza na Wazee wa Zanzibar, Afisi Kuu ya CCM, Kisiwandui, leo Jumapili, Machi 24, 2024, ikiwa ni siku ya pili akiwa kwenye ziara ya kikazi, akitokea Pemba, ambako pia alifanya mazungumzo na mashauriano na Wazee wa Pemba, Jumamosi, Machi 23, 2024.
Amesema, uwepo huo umeondoa hali ya siasa za chuki na uhasama uliokuwepo kabla ya kufikiwa kwa uamuzi wa kuundwa kwake, huku akisisitiza kuwa CCM kitaendelea kutimiza wajibu wake, ili kudumisha umoja na utulivu uliokusudiwa kwa maslahi ya Wazanzibar na Watanzania.
“Binafsi nikimsikia mtu anazungumzia kutaka kujitoa kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa, simwelewi huyo mtu hata kidogo. Kwa sababu Serikali ya Umoja wa Kitaifa ilikuwa kwa ajili ya usalama wa maisha ya watu, usalama wa Wazanzibar, usalama wa Watanzania. Maisha ya watu ni muhimu sana kuliko kitu chochote kwanza. Tuliweka mbele maslahi ya nchi, utulivu na umoja wetu, si vyama vya siasa,” amesema.
Balozi Nchimbi ameongeza kuwa, “mnakumbuka wakati fulani nikiwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, kila siku nenda rudi kwa helkopita kuja Zanzibar. Tulikuwa tunahangaika kuondosha uhasama na chuki. Najua kuna wakati wenzetu wanapata gadhabu na kuzungumza kwa jazba. Sisi wanaCCM tusiende huko hata kidogo.”