Rais wa Klabu Bingwa Tanzania Bara Young Africans, Hersi Said amesema uwezo wa Benchi lao la Ufundi pamoja na ubora wa kikosi walicho nacho msimu huu, vinampa matumaini ya kuibuka na ushindi katika mchezo wao wa Robo Fainali wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns.

Young Africans imepangwa kucheza na miamba hiyo ya Afrika Kusini katika hatua hiyo ambapo mchezo wa mkondo wa kwanza ukipangwa kuchezwa Machi 30 Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam.

Akizungumza jijini Dar es salaam, Rais huyo ameeleza namna ambavyo timu hiyo imepita katika vikwazo vigumu msimu huu chini ya kocha huyo raia wa Argentina, lakini uwezo wake pamoja na kuwatumia vizuri nyota waliopo kwenye kikosi chake vimeweza kuwafikisha hapo walipo.

“Nikweli tunakabiliwa na mchezo mgumu dhidi ya Mamelodi Machi 30, lakini hatuendi kinyonge tunajivunia ubora wa benchi letu la ufundi linaloongozwa na Miguel Gamondi, lakini tuna kikosi bora na imara mno msimu huu, ambacho kimekutana na timu ngumu na kutufikisha hapa kwa hiyo tunaimani tutashinda na kuvuka hatua ya Nusu Fainali,” amesema Hersi.

Kiongozi huyo amesema wakati huu wa maandalizi ya mchezo huo, yeye na viongozi wenzake wapo tayari kutoa msaada kwa Gamondi na wenzake, ili kuwasoma wapinzani wao kama ambavyo wao wamekuwa wakiwafuatilia tangu Droo ilipochezeshwa, lengo ni kuhakikisha wanashinda na kusonga mbele.

Amesema pamoja na ubora wa wapinzani wao lakini lengo lao ni kurudia kile walichokifanya kwa timu ya CR Belouizdad kwenye hatua ya makundi ya kuutumia uwanja wa nyumbarni kupata ushindi wa mabao mengi, ili kujiweka katika mazingira rahisi ya kuvuka Nusu Fainali kweye mchezo wa marudiano.

Young Africans inaendelea na maandalizi yake kambini kwao Avic Town, Kigamboni kujiandaa na mchezo huo ambao unasubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka.

Dkt. Nchimbi: Umoja wa Kitaifa ni maisha ya Watu
Washukiwa shambulio la Urusi wafikishwa Mahakamani