Mradi wa kuwawezesha Wanawake katika mnyororo wa thamani wa mazao ya uvuvi kwa nchi za Afrika Mashariki kupitia Ziwa Victoria umezinduliwa, ili kumuwezesha Mwanamke kuongeza kipato kupitia mazao hayo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa kufunga mafunzo ya siku tatu ya Mtandao wa Wanawake Afrika Wanaojishughulisha na Uchakataji na Biashara ya Samaki (AWFISHNET), uliohusisha Wanawake Viongozi wa mtandao huo kutoka nchi 44 za Afrika, Mkurugenzi wa mradi huo Bi. Suzanne Njeri amesema utatekelezwa katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda.
Amesema, mradi huo wa majaribio utatekelezwa kwa kipindi cha miaka miwili na nusu na mpango ni kuwafikia wanawake 5,000 Afrika Mashariki, ambapo kwa kila nchi watakuwa wanawake 1,667 na kwamba utakuwa na mambo mbalimbali ya kumuwezesha mwanamke lakini kubwa zaidi ni kumuinua mwanamke kuanzia pale alipo ili aweze kuongeza uzalishaji wa mazao ya uvuvi.
Akiiwakilisha Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika hafla hiyo, Afisa Uvuvi Mkuu Bi. Jovice Mkuchu amesema wizara imeweza kufanya tathmini mbalimbali kwenye Sekta ya Uvuvi, ambapo mradi unaenda kutatua changamoto za wanawake katika kupunguza upotevu wa mazao ya uvuvi tangu yanapovuliwa.
Amesema, Wizara inashukuru uwepo wa mradi huo ambao umeona umuhimu wa kuwainua wanawake wa Tanzania katika Sekta ya Uvuvi kwa kuwa wizara ni mlezi wa mtandao wa Wanawake Wanaojishughulisha na Uvuvi Tanzania (TAWFA) na kwamba wizara itakuwa bega kwa bega kuwezesha mradi huo kuwa na tija.
Kwa upande wake Mshauri Mkuu Elekezi wa mradi huo, Editrudith Lukanga amesema mradi unafadhiliwa na taasisi ya Bill and Melinda Gates kwa thamani ya takriban Dola za Kimarekani Milioni 1.5 na utakuwa wezeshi kwa kuwa umewashirikisha wadau kuanzia ngazi ya chini.