Kocha wa Azam FC, Youssouph Dabo, ameanza kuandaa silaha zake za maangamizi kwa ajili ya mechi zilizobaki za Ligi Kuu, akianza kutafuta pointi tatu katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Namungo FC.
Amesema amecheza mechi ya kirafiki dhidi ya Zimamoto FC, kupata utimamu wa mwili na kujiandaa na mechi zinazokuja kwa kuendelea walipoishia katika mechi yao ya mwisho dhidi ya Young Africans ambayo waliibuka na ushindi wa mabao 2-1.
Kocha huyo kutoka nchini Senegal amesema mechi hiyo imemsaidia kuona mapungufu ya kikosi chake na kuyafanyia kazi kwa sababu malengo yao ni kutafuta pointi muhimu katika kila mechi.
Amesema anachoangalia ni umakini wachezaji wake katika kila eneo, safu ya ulinzi na ushambuliaji kuhakikisha wanatumia nafasi zinazopatikana na kutoruhusu bao.
“Mchezo wetu wa kirafiki ulikuwa muhimu sana, hatuangalii matokeo bali ni yale niliyowapa uwanja wa mazoezi, mikakati yangu ni kufanya vizuri katika michezo iliyopo mbele yetu tukianza na dhidi ya Namungo FC” amesema Dabo.
Ameongeza kuwa anafurahi kuona baadhi majeruhi wameanza kurejea kufanya mazoezi mepesi jambo ambalo linampa matumaini ya kurejea kwa kikosi kipana.
“Majeruhi walioanza mazoezi ni beki wetu Sebo (Abdallah Kheri), ameanza mazoezi ya utimamu wa mwili, Sospeter Bajana na Navarro (Franklin) aliyetakiwa kuwa nje kwa miezi minne, ameshatumikia mwezi mmoja amebakiza mitatu kurejea uwanjani.”
Azam FC wanaendelea kujifua katika uwanja wao wa Azam Complex uliopo Chamazi, Dar es Salaam, kujiandaa na mchezo wao dhidi ya Namungo FC utakaopigwa Aprili 13, mwaka huu, kwenye dimba la Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi.